Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Ijumapili alasiri, KM Ban Ki-moon ameripoti kuwa na huzuni kuu juu ya ripoti kuhusu shambulio la gari liliobeba bomu, lilioripiliwa katikati ya mji wa Baghdad, ambapo mamia ya watu waliuawa na kujeruhiwa. Alishtumu vikali vitendo hivi vya kutumia mabavu, kihorera, vitendo ambavyo mara nyingi huwalenga raia na hudhamiria kuchafua juhudi za kurudisha utulivu na amani katika Iraq. KM aliwahimiza umma wote wa Iraq kutunza maendeleo yao ya kisiasa yaliofikiwa nchini kwa sasa, licha ya kuwa wanakabiliwa na matukio ya vurugu la kukirihisha la mara kwa mara, na aliwasihi wasibadilishe tarehe ya kufanyisha uchaguzi ya 16 Januari 2010, na kutarajia upigaji kura utakuwa huru na wa haki.

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti watu 13,800 wanaokimbia mapigano yaliovuma kwenye eneo la Waziristan Kusini, Pakistan wameshasajiliwa hivi sasa na UM, na wamejiunga na watu 85,000 wengine waliokimbia makwao kwenye eneo hilo kuanzia mwezi Juni. Jumla ya watu waliong'olewa makazi kutoka wilaya mbili hizi jirani za kaskazini-magharibi, katika Pakistan, kwa sasa, ni sawa na raia 182,000. UM imeshaandaa mradi wa dharura kuhudumia kihali mmiminiko mpya wa wahamiaji wanaohajiri makwao kwa sababu ya mapigano, na mashirika ya UM pia yapo tayari kukidhi mahitaji ya dharura kwa umma huo. Hivi sasa mashirika ya UM na jumuiya wenzi zinazoshughulikia misaada ya kiutu yameshagawa tani 1,000 za chakula; na watu 30,000 wamefadhiliwa vifaa vya matumizi ya nyumbani, na wakati huo huo watu 35,000 wamepokea vifurushi vya kutunza afya kwa madhumuni ya kuwakinga na hatari ya kuenea kwa maradhi ya kuambukiza kwenye mazingira ya msongomano uliokiuka mipaka. Kadhalika mashirika ya kimataifa yamehakikisha wahamiaji 45,000 wengine wanapatiwa huduma za maji safi na salama kwa matumizi yao ya kila siku.

Ilivyokuwa mwaka 2009 unakaribia kumalizika, Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) katika Afghanistan linajitayarisha kukamilisha mradi wa kuwapatia makazi ya muda zaidi ya watu 50,000 waliorejea nchini katika mwaka huu. Kuanzia 2002 mpaka mwisho wa Septemba 2009 UNHCR imeshawapatia raia wa Afghanistan 190,000, wasiojiweza kihali, waliorejea makwao, msaada wa kupata makazi ya muda, hasa katika vijiji, mradi ambao, kijumla umefaidisha kihali raia milioni 1.2 kote nchini. Wakati huo huo, mnamo 17 Oktoba 2009, serikali ya jimbo katika eneo la Bamyan, kwa msaada kutoka mashirika ya kimataifa, imeanzisha kampeni ya kufundisha kusoma na kuandika kwa wakazi wake kwa matarajio haliya kutojua kusoma na kuandika itafutwa kabisa kieneo katika miaka mitano ijayo.

Alain Le Roy, Naibu KM juu ya Operesheni za UM Kuhusu Ulinzi Amani Ijumanne atafanya safari ya kuzuru Abuja, Nigeria kuhudhuria mkutano maalumu wa wadhifa wa juu, wa Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika. Baada ya hapo Le Roy atazuru operesheni za kulinda amani za UM katika Eneo la Maziwa Makuu - ikijumlisha JKK (DRC) na pia Burundi. Atakapozuru JKK atajumuika kutathminia hali ya usalama katika eneo la mashariki, na kuzingatia namna ya kuzihusisha kikamilifu taasisi muhimu za kiserikali katika ujenzi wa mioundombinu ya amani nchini, kwa ujumla. Wakati atakapozuru Burundi atajaribu kujionea binafsi utekelezaji wa operesheni za pamoja za UM kudumisha amani nchini.

Profesa Frances Stewart amehishimiwa rasmi, mapema wiki hii, na Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) kwa kutunukiwa Zawadi ya Mahbub ul Haq, kwa mchango wake mkubwa katika kustawisha maendeleo ya kijamii kwa umma wa mataifa yanayoendelea. Taadhima ya kumtunza Profesa Stewart zawadi hiyo ilifanyika kwenye mji wa Busa, Jamhuri ya Korea. Profesa Stewart anafundisha somo la uchumi maendeleo katika Chuo Kikuu cha Oxford, Uingereza, na ni miongoni mwa wataalamu mashuhuri wanayehusika na rai ya kupima maendeleo ya wanadamu kwa viashirio vinavyotumiwa na UNDP, kadhia ambayo hujumlishwa kwenye Ripoti ya Maendeleo ya Wanadamu inaotolewa mara kwa mara na UNDP kuanzia 1990.