Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

KM ameamua kumrudisha Peter Galbraith kutoka Afghanistan na kumwachisha madaraka ya Naibu Mjumbe Maalumu wa KM kwa Shirika la Usaidizi Amani la UM katika Afghanistan (UNAMA). Kwenye taarifa aliotumiwa Galbraith na KM, Ban Ki-moon alimshukuru kwa bidii yake kubwa ya kazi na mchango muhimu wa kitaalamu aliojumuisha wakati alipokuwa mtumishi wa kiraia wa kimataifa anayetumikia UM. KM alichukua uamuzi wa kumwachisha kazi Galbraith kwa maslahi bora ya shirika la UNAMA. KM alikariri kuunga mkono moja kwa moja kazi za Mjumbe Maalumu wa UM kwa Afghanistan, Kaie Eide.

KM amesikitishwa sana na madhara yaliotukia kwenye maeneo ya Samoa, Samoa ya Marekani na Tonga baada ya zilzala na mawimbi ya tsunami kupiga huko, na kugharikisha maisha mnamo tarehe 29 Septemba, na kusababisha vifo vyingi, mamia ya majeruhi na uharibifu mkubwa wa mali. KM ameripotiwa kufuatilia, kwa ukaribu zaidi, tukio hili na vile vile athari za tetemeko la ardhi liliotukia karibu na Sumatra magharibi. Aliwatumia salamu za pole jamii za watu waliouawa na ajali hizi, na pia majeruhi na wale waliokosa makazi kwa sababu ya maafa. Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imetuma timu ya dharura Samoa kutahminia mahitaji ya kupelekwa huko kuhudumia kihali waathirika husika. Hivi sasa UM una wasiwasi ya kuzuka upungufu wa chakula katika visiwa vya Tonga na Samoa, pamoja na ukosefu wa wahudumia afya wanaotakikana kutibu umma majeruhi. Shirika la Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) sasa hivi linafanya mapitio ya vifaa vinavyohitajika kwenye sekta ya afya, ili kuhudumia mazingira ya usafi na maji safi na salama.

Ripoti mpya ya KM juuya Cote d'Ivoire inaeleza kwamba baada ya kumalizika operesheni za kusajili utambulisho na orodha ya wapiga kura nchini, taasisi za kitaifa kwa sasa zinakabiliwa na jukumu kubwa la kukamilisha utaratibu wa uchaguzi kwa bidii zaidi na kutayarisha upigaji kura usio na shaka, ulio huru, wa haki na wenye uwazi unaoaminika. Hali hii, aliongeza kusema, itahitajia kuchapishwa orodha kamili ya mwisho ya wapiga kura inayoridhisha. Ripoti ilieleza ya kuwa uhalali wa utaratibu unaoandaliwa wa kuendesha uchaguzi utategemea namna mizozo itakayozuka baada ya kuchapishwa orodha ya muda ya wapiga kura itakavyoshughulikiwa na wenye mamlaka. Ripoti ilionya pindi utaratibu huo hautosimamiwa sawasawa na kwa uwazi unaoridhisha, shuguhuli za uchaguzi huenda zikawa ndio chanzo cha kuzusha hali ya kigeugeu na vurugu. Viongozi wa Cote d'Ivoire walinasihiwa na KM kwenye ripoti yake kutekeleza ahadi zao za kusimamia uchaguzi bila ya matatizo, kwa imani ya kuvumiliana, kwa kuonyesha mapatano na kuhakikisha raia wanajumuishwa kwenye shughuli za serikali zao.

Ripoti nyengine ya KM iliowakilishwa wiki hii inahusika na hali ya usalama katika JKK. Ripoti ilieleza kwamba maendeleo ya eneo hilo hayajalingana katika usawazishaji wa utulivu kwenye sehemu ya mashariki. Kumekutikana kuwepo makundi ya watu wenye silaha ambayo hayajajiunga bado na jeshi la taifa, ilisema ripoti, wakati baadhi ya makundi yamekutikana kujitenga kabisa na utaratibu wa kusalimisha silaha na kujiunga na jeshi la taifa. Kadhalika, makundi hayo mara nyengine yalikutikana kujiunga na waasi wa kundi la Kihutu la FDLR wanaopigana na vikosi vya Serikali. Tatizo hili, alisema KM, linachochewa na kuzorota kwa utekelezaji wa Maafikiano ya Amani ya Mwezi Machi. Majukumu yanayotakikana kutekelezwa ili kurudisha amani kwa sasa, ilisisitiza ripoti, hasa katika eneo la mashariki ni magumu. Miongoni mwa matatizo yanayozorotisha shughuli za kurejesha amani hujumlisha ukiukaji wa haki za kibinadamu unaoendelezwa na makundi ya mgambo yenye silaha, na pia athari haribifu kwa raia za zile operesheni za kijeshi za vikosi vya Serikali dhidi ya waasi Wahutu wa Rwanda.