Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kilimo katika Afrika kinaashiria maendeleo ya kuridhisha, inasema FAO

Kilimo katika Afrika kinaashiria maendeleo ya kuridhisha, inasema FAO

Ripoti ya makala ya kujadiliwa, iliochapishwa hii leo na Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) imeeleza kwamba utendaji hakika, wa kutia moyo, ulioshuhudiwa kufanyika hivi karibuni kwenye sekta ya kilimo katika zile nchi za Afrika ziliopo kusini ya eneo la Jangwa la Sahara, umebainisha utengano halisi na tabia za kikale, zilizopitwa na wakati, za kilimo, na kuwakilisha mwelekeo mpya wenye matarajio ya ukuzaji kilimo maridhawa kieneo, maendeleo yatakayokuwa na natija kubwa kwa umma, kwa ujumla.

Hata hivyo, ripoti ilisema bado kutahitajika "sera za utendaji wa pamoja zenye madhumuni maalumu" ya kudumisha kasi ya maendeleo haya. Baada ya kupita miongo kadha ambapo maendeleo ya kilimo yaliporomoka katika mataifa nchi za kusini mwa Sahara - ambapo asilimia 80 ya sekta hiyo hujumlisha wakulima wadogo wadogo - ilidhihirika katika 2008, sekta ya kilimo ilionyesha ukuaji wa haraka wa asilimia 3.5, kuzidi kile kima cha asilimia 2 kinachowakilisha ongezeko la idadi ya watu. Juu ya hayo, ripoti ilibainisha vizingiti kadha kusalia bado, ambavyo huzorotesha maendeleo ya kilimo, na ambavyo vinatakikana kushughulikiwa kipamoja na serikali, wafadhili wa kimataifa na sekta ya binafsi ili kuimarisha sekta ya kilimo katika mataifa ya kusini ya Sahara, na kuhakikisha maendelo ya kilimo yanalingana na kadhia ya kupunguza umaskini na hali duni kwenye sehemu hizi za Afrika. Miongoni mwa matatizo hayo hujumuisha mzoroto katika fungamano za kikanda kwenye maendeleo ya vijijini, upungufu wa utawala bora, na taasisi dhaifu za kuongoza shughuli za kiserikali kwenye baadhi ya mataifa husika, ikichanganyika na hali ya kuselelea kwa mapigano na vurugu, na miripuko ya maradhi maututi, mathalan, maambukizi ya VVU na UKIMIWI wenyewe. Vile vile kuna shida bado za kuwaunganisha wakulima wadogo wadogo na soko za kitaifa na kimataifa, hali ambayo ikitekelezwa kama inavyotakikana, itasaidia sana kuzalisha fursa za watu kupata ajira katika maeneo ya vijijini na kuwapatia vijana pia mafunzo yanayotosheleza kuhudumia maisha.