Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti za UM zinasema, inayumkinika makosa ya vita yalitendeka katika JKK

Ripoti za UM zinasema, inayumkinika makosa ya vita yalitendeka katika JKK

Ripoti mbili zilizotayarishwa bia na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu pamoja na Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani katika JKK (MONUC), na kuwasilishwa siku ya leo, zinasema inayumkinika vitendo vya makosa ya jinai ya vita, vikichanganyika na uhalifu dhidi ya utu, viliendelezwa kwenye eneo la mashariki la JKK.

Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu, Navi Pillay alieleza Ijumatano kwamba ripoti hizi mbili zimethibitisha kihakika kwamba mfululizo wa vitendo vilivyokiuka haki za kiutu, viliotukia kwenye eneo la mashariki katika JKK, vinahitajia mchango muhimu wa dharura, kutoka serikali ya JKK pamoja na jumuiya ya kimataifa, ili kudhibiti madhila kama haya yasiibuke tena. Ripoti zimependekeza kuanzishwe "marekibisho ya kimsingi" kwenye mifumo yote ya mahakama na kanuni za usalama katika JKK. Uchanganuzi wa ripoti ulizingatia mfululizo wa matukio yalioyavaa majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini katika kipindi kilichoanzia miezi ya Oktoba mpaka Novemba 2008, wakati ambapo mapigano makali yalivuma baina ya vikosi vya serikali vya FARDC na majeshi ya mgambo ya CNDP, ambayo wakati huo yaliongozwa na Laurent Nkunda.