Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

KM Ban Ki-moon, kwa kupitia msemaji wake, aliripotiwa kuupongeza umma wote wa Afghanistan - wanaume na wanawake - kwa kutekeleza haki yao ya Kikatiba na kupiga kura kwenye uchaguzi rasmi wa Uraisi na Baraza la Wawakilishi wa Majimbo, uliofanyika siku ya leo, tarehe 20 Agosti. Alisema kitendo hiki kimemthibitishia dhahiri matakwa ya umma wa Afghanistan ni kurudisha utulivu nchini mwao na kuimarisha maendeleo yenye natija kwa wazalendo wote.

Mjumbe Maalumu wa KM kwa Afghanistan, Kai Eide, yeye kwa upande wake aliripotiwa kuzuru moja ya vituo vya kupigia kura katika mji wa Kabul mnamo kati ya siku ya leo. Aliwaambia waandishi habari mjini Kabul kwenye mazungumzo nawo kwamba aliingiwa moyo kuona uchaguzi umefanyika nchini, na kulitukia fujo chache sio kama ilivyodhaniwa hapo kabla. Uchaguzi wa Afghanistan, alisisitiza, ulikuwa ni hatua muhimu sio kwa raia tu bali pia wadau wa kimataifa wanaohusika na maendeleo nchini humo. Aliongeza kusema matayarisho ya uchaguzi yalikuwa magumu kwa kila njia, kwa sababu ya miundombinu dhaifu, taasisi dhaifu za kuendesha shuguhuli za utawala, pamoja na masafa marefu ya kufikia vituo vya yale maeneo yaliopo mbali na miji ikichanganyika na vizingiti kadha wa kadha vyenginevyo. Kwa kulingana na bayana hii alisema ana hishima kuu kwa ujasiri wa umma wa Afghanistan kuvumilia hali ya mkorogano na kuweza hata kushiriki kwenye upigaji kura wa taifa.

Asubuhi Baraza la Usalama lilifanya mashaurinao juu ya Lebanon na Sudan. Kuhusu Lebanon, Edmond Mulet, Katibu Mkuu Msaidizi juu ya Operesheni za Ulinzi Amani za UM alihutubia Baraza kuhusu opersheni za Vikosi vya UM vya Uangalizi wa Muda katika Lebanon (UNIFIL). Vile vile alisailia ripoti ya KM kuhusu maandalizi ya uchaguzi ujao wa katika Sudan. Kadhalika, Mwakilishi wa Uturuki, mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Usalama kuhusu azimio 1718 aliwasilisha ripoti yao juu ya maendeleo kwenye utekelezaji wa vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Umma wa Korea (DPRK).

Kundi la Ushauri kwa KM juu ya Nishati na Mabadiliko ya Hali ya Hewa limekutana mjini Stockholm Alkhamisi, kwenye kikao cha pili na kujadilia mapendekezo ya sera zilizolenga matumizi ya nishati kwa ufanisi, na uwezo wa mataifa kupata nishati ya kuridhisha. Taarifa iliotolewa na tume hii inasema mada mbili hizi ni masuala muhimu kabisa yenye kuhitajia usikivu wa makini kwenye juhudi za kujadilia udhibiti bora wa athari za mabadiliko ya hali ya hewa. Kikao cha kwanza cha Kundi la Ushauri kilifanyika 17 Juni 2009 mjini New York pale tume ilipoanzishwa rasmi, tume ambayo hujumlisha viongozi wafanyabiasahara, wataalamu na watu wanaohusika na shughuli za nishati na inaoongozwa na Kandeh Yumkella, Mkurugenzi wa Shirika la UM juu ya Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) na Mwenyekiti wa Taasisi ya Nishati kwa UM.