Skip to main content

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) limeripotiwa kuingiwa wasiwasi mkuu juu ya kuharibika kwa hali ya usalama Yemen, hususan athari zake kwa watoto wadogo na wanawake - kufuatia mifumko ya vurugu lilionea katika eneo la kaskazini ya nchi. Kwa mujibu wa taarifa za UNICEF watu 100,000 wameathirika na mgogoro huo, asilimia kubwa yao wakiwa watoto. UNICEF imeripoti imeshaanzisha kugawa vifaa vya kuchujia maji pamoja na majerikeni ya maji, na zana za huduma ya afya, na vile vile imegawa tembe 300,000 za kusafishia maji. Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) sasa hivi linajiandaa kupeleka misaada ziada ya chakula kwa watu 150,000 katika Yemen baada idadi yao kuongezeka kutoka mwezi uliopita. Shirika la UM linaloshughulikia huduma za wahamiaji, yaani UNHCR, limeeleza ya kwamba katika wiki mbili zilizopita watu 35,000 waling\'olewa makazi kutokana mapigano yaliopamba kaskazini katika Yemen. Wakati huo huo, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeripoti kwamba aila nyingi za wahamiaji wa ndani Yemen wameonekana kuambukizwa na malaria, na wengine wanasumbuliwa vile vile na maradhi ya kuharisha na mapele ya mwili.

Dktr Margaret Chang, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) akijumuika na Mjumbe Maalumu wa KM Kudhibiti Malaria, Ray Chambers hii leo wameripotiwa kutembelea Uganda. Dhamira hasa ya ziara yao - ambayo vile vile iliwafikisha Tanzania - ilikuwa ni kufanya mapitio kuhusu maendeleo kwenye zile bidii za kudhibiti malaria, na kujaribu kuelewa vyema matatizo yalioselelea kwenye zile sehemu zenye kuathirika sana na malaria. Wakuu hawo, yaani Chambers na Chan, walipokuwa Uganda walikuwa na mazungumzo na wataalamu wazalendo wanaohusika na malaria, na pia walishauriana na viongozi wa serikali baada ya kumaliza ziara ya vituo vya afya vya katika miji na vijiji. Kadhalika, mnamo mwanzo wa wiki Mkuu wa WHO na Mjumbe wa KM juu ya Udhibiti wa Malaria walikutana na Raisi Jakaya Kikwete wa Tanzania. Waliripoti kwamba lengo hasa la huduma zao za muda mrefu ni kuhakikisha vifo vya malaria vitakomeshwa, kwa kuambatana na pendekezo la KM la kuzipatia nchi zote zilizoathirika na malaria udhibiti bora wa ugonjwa huo itakapofika 2010. Raisi wa Mradi wa Afya ya Kimataifa katika Taasisi ya Wakf wa Bill na Melinda Gates naye vile vile alijiunga na Chambers na Chan kwenye safari yao.

Shirika la UNICEF hivi sasa limeanzisha mradi wa kugawa vyandarua 59,000, kwa kupitia mashirika ya kienyeji, katika wilaya ya Sakow, Juba ya Kati na kwenye sehemu ya Wanla Weyne, maeneo yaliopo kusini-kati nchini Usomali. Kadhalika mnamo wiki iliopita watoto 5,000 baina ya umri wa miezi 6 mpaka 36, kwenye Wilaya ya Weyne, walipatiwa vyakula vilivyopikwa tayari na vyenye virutubisho vya kuwakinga na hatari ya utapiamlo mbaya. Halkadhalika, Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) likijumuika na makundi ya kienyeji limekamilisha mradi wa kugawa chakula katika Puntland, Usomali, mradi uliofanikiwa kuwapatia watoto 17,000, chini ya miaka mitano, msaada huo wa kunusuru maisha. Vile vile katika mji wa bandari wa Bossaso, Puntland shirika la UM juu ya huduma za wahamiaji (UNHCR) limeanzisha mafunzo maalumu kwa mamia ya raia wanaofikiria kuhama nchi kuelekea Yemen kutafuta maisha bora, kwa kutumia mashua za magendo za kuwavusha kwenye Ghuba ya Aden. Mnamo wiki hii UNHCR imegawa vipeperushi makhsusi vyenye maelezo sahihi yanayohadharisha hatari ya safari za magendo za kwenda Yemen ambapo katika miaka ya karibuni wahamiaji wingi walipoteza maisha, ama kwa kuzama baada ya kutupwa majini na wafanya magendo au pale mashua zao zinapopinduka.