Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNICEF kuzuru JKK wiki ijayo kusailia jinai ya kijinsiya

Mkuu wa UNICEF kuzuru JKK wiki ijayo kusailia jinai ya kijinsiya

Ann Veneman, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) wiki ijayo, anatarajiwa kufanya ziara ya siku tano katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK).

Mara ya mwisho Veneman alizuru JKK ilikuwa ni mwezi Februari mwaka huu. Mkurugenzi wa UNICEF anatazamiwa kutembelea Kinshasa na Kivu ya Kaskazini na atakapokuwepo huko atakutana na familia na aila mbalimbali, pamoja na watoto waathirika wa jinai ya kuingiliwa kimabavu, na atakutana pia na zila aila ambazo watoto wao walitoroshwa na majeshi ya mgambo na vile vile kukutana na familia zilizong'olewa makazi kwa sababu ya mapigano. Kwa mujibu wa taarifa ya UNICEF, Veneman atakapoonana na wawakilishi wa Serikali, na wale wa mashirika ya UM katika JKK pamoja na watumishi wa mashirika yasio ya kiserikali, watajaribu kuzingatia namna ya kuimarisha miradi ya kitaifa na kikanda, kwa makusudio ya kuzihifadhi aila hizo waathirika pamoja na watoto wao dhidi ya jinai ya vita na unyanyasaji wa kijinsiya unaoendelea kufanyika kwenye JKK.