Hapa na Pale

Hapa na Pale

KM Ban Ki-moon ameshtumu, kwa kauli kali kabisa, shambulio la kujitoa mhanga liliotumia gari, na kutukia Ijumamosi kwenye sehemu ya kati ya mji wa Kabul, ambapo watu saba wanaripotiwa waliuawa na idadi kubwa ya watu walijeruhiwa, ikijumlisha mfanyakazi mmoja wa UM. Taarifa ya KM ilisema ameingiwa wahka juu ya usalama nchini kwa sababu ya kuzuka kwa vurugu la kihorera, siku chache tu kabla ya Uchaguzi wa Raisi na Majimbo, unaotarajiwa kufanyika tarehe 20 Agosti (2009). KM aliwatumia mkono wa taazia na pole kwa aila zote za waathiriwa wa tukio hilo. Kadhalika aliwatumia aila za majeruhi salamu za kuwaombea wapone haraka.

Mkutano wa Tunza wa 2009 kwa Watoto na Vijana wa Kimataifa kuhifadhi mazingira, umeanza majadiliano ya wiki moja Ijumatatu katika mji wa Korea ya Kusini wa Daejeon. Kwenye mkutano huo wamekusanyika vijana 800 ziada kutoka nchi zaidi ya 100 kusailia taratibu za kuhamasisha serikali zao "kufikia makubaliano ya majadiliano" yanayoridhisha, kwenye Mkutano Mkuu wa Copenhagen, utakaofanyika mwezi Disemba, kuzingatia mabadiliko ya hali ya hewa. Vijana hawa wanapendekeza serikali zao zifikie haraka maafikiano mapya, yanayoaminika kisayansi, na yenye natija za muda mrefu kwa ulimwengu mzima. Mkutano wa Daejeon umetayarishwa na Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP), na ni miongoni mwa zile kampeni zinazotumiwa na KM kuhamasisha imani ya kisisia kimataifa pamoja na mchango wa umma, utakaowasilisha mapatano ya jumla juu ya udhibiti bora wa athari za mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni.

Balozi Caroline Millar wa Australia, aliye Raisi wa Mkutano wa Kuondosha Silaha Ulimwenguni, unaofanyika Geneva, alinakiliwa akisema ya kwamba katika kipindi cha sasa hivi haitowezekana kuwa na muafaka juu ya utekelezaji wa ratiba ya kazi za Mkutano. Mataifa ya Uchina na Iran yalimshukuru Raisi wa mkutano kwa juhudi zake na mashauriano alioyaendeleza na wajumbe wa kimataifa, mashauriano yaliokuwa na uwazi wa kuridhisha ya kutaka kuleta maafikiano juu ya ratiba ya kazi. Uchina na Iran yameahidi kuwa yataendelea kuunga mkono juhudi za Raisi wa Mkutano wa Kuondosha Silaha Ulimwenguni ili wajumbe waanze shughuli zao haraka iwezekanavyo.

Njia za kufikia na kupata maji safi, zinazidi kuwa ngumu kila mwaka kwa sababu ya kuongezeka kwa mahitaji ya maji kwa umma wa kimataifa, ikichanganyika na upatikanaji wa maji yasio salama yenye kuhatarisha raia wa kimataifa. Takwimu za UM zinakadiria watu bilioni moja, yaani sawa na sehemu ya sita ya idadi ya watu duniani, huwa na upungufu mkubwa wa maji safi na salama. Kutokana na sababu hizo ndio jumuiya ya kimataifa ilianzisha Wiki ya Maji Safi Duniani, wiki ambayo huadhimishwa kila mwaka baina ya tarehe 16 mpaka 22 Agosti, na hutumiwa kama ni jukwaa la kuwajumuisha viongozi wa dunia na wataalamu wa sayansi ya maji kubadilishana suluhu bunifu juu ya masuala yanayohusu namna ya kupata maji safi na salama kwa umma wa kimataifa, na kudhibiti athari zake kwenye hali duni ya umaskini, afya bora, ilimu, usawa wa kijinsiya na mazingira safi. Taadhima za 2009 zimeandaliwa na Taasisi ya Maji Kimataifa ya Stockholm, na lengo lake safari hii ni kujenga uwezo wa watu kupata maji safi, na kuendeleza ushirikiano wa kimataifa, pamoja na kufanya mapitio ya maendeleo yaliofikiwa hivi sasa ulimwenguni kwenye kadhia hizo. Mada ya Wiki ya Maji Safi kwa 2009 ni : "Tukabiliane na Vizingiti vya Kimataifa: Tufikie Maji Safi na Salama kwa Natija za Umma - Hasa Maji Yaliovuka Mipaka." Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) limeandaa warsha kadha wiki hii, zitakazozingatia afya bora, kwa watoto, usafi na afya bora katika maskuli.

KM amemteua Judy Cheng-Hopkins wa Malaysia kuwa KM Msaidizi juu ya Operesheni za Ujenzi wa Amani na atamrithi Jane Holl Lute wa Marekani, ambaye ameutumikia UM tangu 2003. Bi Cheng-Hopkins ana uzoefu wa miaka 30 kuhudumia mashirika mbalimbali ya UM, ambapo alifanya kazi na mashirika yanayohusu masuala ya kiutu, na kwenye maeneo yanayoibuka kutoka mapigano na uhasama, na vile vile alishughulikia huduma za ujenzii wa amani na utulivu, pamoja na kuhudumia masuala yanayohusu maendeleo. Uzoefu huu unamfanya Cheng-Hopkins kuwa mtaalamu mwenye uwezo wa kusukuma mbele, kwa mafanikio, ajenda ya KM ya kurudisha tena utulivu na amani kwenye maeneo yalioshuhudia uhasama na mapigano. Karibuni Cheng-Hopkins alikuwa Kamishna Mkuu Msaidizi wa Wahamiaji, akisismamia operesheni za wahamiaji katika nchi 118 duniani.