Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Raisi Barack Obama wa Marekani alipohutubia Baraza Kuu la UM aliwaambia wajumbe wa kimataifa kwamba taifa lake lipo tayari kuanzisha mlango mpya kwenye uhusiano wa kimataifa na nchi wanachama. Aliyataka mataifa yajihusishe kwenye awamu yenye lengo la kukidhi masilahi ya pamoja ya umma wote wa dunia, na kwenye mazingira ambapo mataifa yatahishimiana. Aliutaka ulimwengu kuongeza juhudi zao, mara mbili zaidi, zitakazohakikisha UM utatumiwa kama ni kipengele muhimu cha kuendeleza masilahi ya pamoja ya umma wote wa ulimwengu. Alisisitiza kwamba ukubwa wa matatizo yalioukabili ulimwengu sasa hivi, bila shaka yanahitajia mchango wa Mataifa Wanachama yote, mchango utakaoipa taasisi ya UM maana hakika ya jina lake, kama ni taasisi inayosimamia masilahi ya Mataifa Yalioungana. Alisema mwelekeo huo ndio Marekani ungelipendelea kuuona unatumiwa kuendeleza uhusiano wa kimataifa katika siku za baadaye - hali itakayokuwa ya amani na yenye ustawi, ambayo walimwengu wote wanaweza kuifikia, tukitambua kwamba kila taifa lina haki na dhamana ya kutekeleza majukumu hayo. Makubaliano haya, alitilia mkazo, ndio yenye uwezo wa kuyafikia malengo yanayoridhisha katika uhusiano wa kimataifa.

KM wa UM ametangaza kuwa ana wasiwasi mkubwa juu ya ripoti alizopokea kuhusu mapigano ya karibuni baina ya vikosi vya Serikali ya Sudan na makundi ya waasi, mapigano yaliosababisha maisha ya raia kupotea pamoja na mali kuangamia kwenye eneo la Korma, Darfur Kaskazini. KM ametoa mwito unaoyataka makundi yote husika kuonyesha uvumilivu mkubwa baina yao, na kusimamisha tena mapigano haraka iwezekanavyo, na bila ya shuruti, na pia kuongeza mardufu juhudi za kufikia mapatano ya kisiasa kuhusu mzozo wa Darfur. Alirudia tena umuhimu wa kuhakikisha kunakuwepo ushoroba ulio salama na huru, utakaowawezesha wahudumia misaada ya kiutu na watumishi wa UM kulifikia lile eneo la uhasama, ili kuchunguza hali halisi ilivyo kwenye uwanja wa mapigano, na kuhudumia mahitaji ya kunusuru maisha kwa umma husika.

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limesimamisha, kwa muda, operesheni zake za kugawa chakula kwenye eneo liliokaribiana na Adilla, katika Darfur Kusini, baada ya magari yake mawili yaliokuwa yamebeba chakula chenye uwezo wa kuhudumia watoto 10,000 kuibiwa. WFP ilisema maofisa wa Serikali ya Sudan walifanikiwa kuwaaminisha wale waliowateka nyara madereva wawili wa magari ya WFP kuwaachia, lakini wajambazi walikataa kuyatoa magari waliyoyaiba. Vikosi vya Mchanganyiko vya UM/UA kwa Darfur (UNAMID) vimetangaza kuwa watafuatilia uchungizi wa tukio hili kwa ukaribu zaidi.

Shirika la UM Kulinda Amani katika JKK (MONUC) Ijumanne limeanza kuwahamisha kutoka Kinshasa, na kuwapeleka Bukavu, waliokuwa waasi, na kuwaunganisha na jeshi la Serikali baada ya kusamehewa na wenye mamlaka. Waasi 122 waliokuwa kizuizini ni wafuasi wa lile kundi la CNDP (National Congress for the Defense of the People). Mjumbe Maalumu wa KM katika JKK, Alan Doss alisema hatua hii itasaidia kujenga hali ya kuaminiana baina ya Serikali na kundi la CNDP.

Ijumatano kulichapishwa ripoti mpya ya KM juu ya ulinzi wa watoto kwenye mazingira ya mapigano nchini Uganda. Ndani ya ripoti KM alikumbusha kwamba waasi wa LRA bado wanaendelea na vitimbi vyao haramu na katili kwenye maeneo jirani, nje ya Uganda. KM amewataka waasi wa LRA kuwasiliana na watumishi wakazi wa timu ya UM, waliopo kwenye maeneo hayo na kuwakabidhi, bila ya kuchelewa, wale watoto waliowakamata kimabavu kupigana na vikosi vyao. Kadhalika, Serikali ya Uganda imetakiwa kuhakikisha wanawapatia watoto ulinnzi imara pale majeshi yao yanapoendeleza operesheni za kijeshi dhidi ya wafuasi wa LRA katika Uganda au pale wanapofanyisha operesheni hizo pamoja na vikosi vya mataifa jirani.

Bodi la Utendaji la Shirika la UM juu ya Ilimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) imemteua Irina Gueorguieva Bokova wa Bulgaria kuwa Mkurugenzi Mkuu mpya, uteuzi ambao untarajiwa kupitishwa kwenye kikao cha Mkutano Mkuu wa UNESCO, katika tarehe 15 Oktoba 2009. Pindi wajumbe wa mkutano wataidhinisha uteuzi huo, Bi Bokova atakuwa mwanamke wa kwanza kihistoria kuongoza shughuli za UNESCO. Bokova, Balozi wa Bulgaria katika Ufaransa na Mjumbe wa Kudumu katika UNESCO aliteuliwa kuongoza UNESCO kati ya wagombania tisa walioshiriki kwenye upigaji kura wa duru tano wa Bodi la Utendaji wa UNESCO.