Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Raisi mstaafu wa Marekani Bill Clinton, Ijumatatu, tarehe 06 Julai atafanya ziara ya awali katika Haiti, kama Mjumbe Maalumu wa KM kwa taifa hilo. Atakapokuwepo Haiti atakutana kwa mashauriano na maofisa wa Serikali juu ya namna ya kulisaidia taifa kujiandaa vizuri zaidi kukabiliana na matatizo ya vimbunga, kuzalisha ajira mpya na kuimarisha huduma za kimsingi za jamii. Clinton pia atajadilia taratibu za kufungamanisha shughuli za UM, jumuiya za kiraia na jamii ya wafadhili wa misaada ya maendeleo na miradi ya Serikali katika kufufua huduma za uchumi na jamii.

Msemaji wa KM ametangaza kwamba Ban Ki-moon ana wasiwasi kuhusu mzozo wa kisiasa na kikatiba unaoendelea katika Niger hivi sasa, ambao unahatarisha utulivu nchini na kudhoofisha maendeleo yaliofanyika miaka ya karibuni, ya kuimarisha utawala wa kidemokrasia na kuhishimu sheria za taifa. Alisema anasikitika na uamuzi uliochukuliwa majuzi na Serikali ya Niger, uliozusha ugumu mkubwa kwenye zile kazi za taasisi za kidemokrasia na Mahakama ya Katiba, kutekeleza majukumu yao kama wadhamini watakaosimamia raia kufuata sheria za nchi. KM ametoa mwito unaopendekeza makundi yanayohasimiana yawe na uvumilivu miongoni mwao na kusuluhisha mifarakano yao kwa mazungumzo.

KM amekaribisha na kupongeza ile Taarifa ya Pamoja iliotiwa sahihi kwenye mji wa Sirte, Libya Ijumaa baina ya Serikali za Ghana na Gambia, ili kuhitimisha hali ya wasiwasi iliojiri baina yao baada ya vifo na kupotea kwa raia wa Ghana waliokuwepo Gambia katika 2005. KM aliyapongeza mataifa haya mawili ya Afrika Magharibi kwa kujihusisha kidhati kwenye jitihadi za kusuluhisha tofauti zao kwa nia za amani na kwa kupitia majadiliano. Kadhalika KM alieleza mchango wa Jumuiya ya Maendeleo ya Uchumi kwa Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) ulikuwa ni muhimu sana, pamoja na ushirikiano wao na UM, katika kutatua mfarakano wa Ghana na Gambia.

Ripoti ya KM kuhusu shughuli za Ofisi ya UM kwa Afrika Magharibi (UNOWA), juu ya nusu ya kwanza ya mwaka, iliotolewa wiki hii, ilieleza kwamba hali ya usalama na amani Afrika Magharibi, kwa ujumla, inaendelea kutengenea lakini ni dhaifu sana kwenye sehemu za utawala. KM alielezea wahka juu ya miripuko ya mageuzi ya kiserikali yasio ya kikatiba kwenye eneo hilo. KM alipendekeza "tabia ya kubadilisha serikali, kwa kupitia mapinduzi, inaweza kudhibitiwa pindi jamii ya kimataifa itajibisha vitendo kama hivi, kwa kuonyesha msimamo imara wa pamoja, na usioregarega, katika kukabiliana na vyanzo na matendo yanayochokoza na kuchochea hali hii kuzuka. Masuala mengine yalioangazwa kwenye ripoti yanahusu biashara haramu ya madawa ya kulevya, uhalifu wa mipangilio katika mataifa ya eneo, juhudi za kubashiria migogoro na kuizuia kabla haijafumka, kwa kukuza ushirikiano kati ya taasisi za UM, ECOWAS na Umoja wa Afrika (UA).

Kitengo cha Ushauri wa Masuala ya Kijinsiya cha Shirika la Mchanganyiko la UM-UA kwa Darfur (UNAMID), kwa ushirikiano na Wizara ya Masuala ya Jamii ya Darfur Kaskazini wameanzisha pamoja vituo vya kuhudumia masuala yanayowahusu wanawake waliopo kwenye kambi ya wahamiaji wa ndani ya Abou Shouk katika El Fasher. Vituo hivi vitasaidia kuwapatia kazi na kuwasaidia wanawake kujikinga na udhalilishaji wa kijinsia na vitendo vya kutumia mabavu dhidi yao, na kuwapatia mafunzo ya huduma bora za uzazi.

Jumuiya Mashirika ya UM dhidi ya UKIMWI (UNAIDS) imepokea, kwa moyo mkuu, uamuzi wa Bara Hindi (India) kufuta ile sheria ya kufanya ukhanithi, ubasha na usagaji kuwa ni uhalifu. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa UNAIDS, Michel Sidibé "Mahakama Kuu ya Delhi imerudisha tena hishima na haki za binadamu za mamilioni ya wanaume wenye kujamiana na wanaume wengine, na makuntha (transgendered people) waliobadilisha jinsiya katika Bara Hindi." Alisema sheria zinazokandamiza, kama zile ziliofutwa hivi sasa katika Bara Hindi, kuhusu misenge na wasagaji, huwafanya watu husika kujificha na kuendeleza vitendo vyao nje ya sheria, na kuongeza ugumu kwenye zile huduma za kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi vya UKIMWI miongoni mwa raia, na katika kuwauguza wagonjwa wa maradhi hayo.