Skip to main content

Wamaasai wa Kenya wanatazamiwa kuhifadhi mila za kijadi kwa msaada wa WIPO

Wamaasai wa Kenya wanatazamiwa kuhifadhi mila za kijadi kwa msaada wa WIPO

Mnamo mwisho wa Julai, kwenye sherehe ya jumuiya, iliofanyika chini ya kivuli cha mti wa mkangazi, na kuhudhuriwa na wenyeji wa asili 200, Chifu Kisio na wazee wengine wa Jumuiya ya Wamaasai wa Il Ngwesi, Laikipia, Kenya walikabidhiwa rasmi vifaa vya mawasiliano ya kisasa, vya kurikodia na maofisa wa Shirika la UM juu Ya Hakimiliki za Taaluma Duniani (WIPO).

Vifaa hivi vilikusudiwa kuwasaidia Wamaasai kukusanya na kutunza mirathi tajiri ya utamaduni wao. Ripooti yetu wiki hii itasailia, kwa ufupi, kadhia hii.

Mradi wa mwongozo, wa kihistoria, unaoitwa Mradi Bunifu wa Kutunza Mila ulianzishwa na Shirika la WIPO, kwa lengo la kuwasaidia wenyeji wa asili wa Ki-Maasai kukusanya na kutunza mirathi ya jadi, na wakati huo huo kuwawezesha kudhibiti vyema hakimiliki ya rasilmali yao hii kitaaluma. Kadhalika, WIPO inatarajia huduma za kuhifadhi utamaduni wa asili na mila za wa WaMaasi, kwa kuziorodhesha kwenye vyombo vya mawasiliano ya kisasa, utawasaidia jamii hii ya Kenya kujiepusha na unyonyaji wa mila zao, na pia kuwakinga na utumiaji wa ovyo wa mirathi nje ya makabila yao, vitimbi ambavyo huendelezwa na yale makundi yalionuia kuutumia utamaduni huo kufanya pesa bila ya ridhaa ya jamii husika. Shirika la WIPO vile vile limechukua jukumu la kuwafunza jamii ya WaMaasai wa Il Ngwesi namna ya kutumia na kuhudumia vyombo vya mawasiliano ya kisasa, na kuwaongoza kukinga hakimiliki ya utamaduni wao dhidi ya unyoyaji usiotakiwa. Mradi huu wa WIPO katika Laikipia, Kenya utasaidia kufufua maendeleo ya kiuchumi na kitamaduni kwa WaMaasai wa huko na, hatimaye, kuwajumuisha kwenye natija za mawasiliano ya kisasa, yanayolingana na nasaba zao, na ya bila ya makandamizo ya maisha ya kisiku hizi.

Mafunzo ya mradi wa kudhibiti mila na tamaduni za asili za Wamaasai wa Laikipia, Kenya yanasimamiwa na WIPO, kwa ushirikiano na Taasisi ya Marekani juu ya Mila za Jamii pamoja na Chuo Kikuu cha Duke kiliopo Marekani.

Nikiripoti kutoka Makao Makuu ni AWK, wa Idhaa ya Kiswahili ya Redio ya UM, NY.