Skip to main content

Hapa na pale

Hapa na pale

Ripoti mpya ya KM kuhusu maandalizi ya uchaguzi katika Sudan, uchaguzi unaotazamiwa kufanyika mwezi Aprili 2010, imeeleza kwamba ijapokuwa kumepatikana mafanikio ya kutia moyo kwenye matayarisho ya jumla, hata hivyo, hatua chache za kimsingi zimesalia kutekelezwa na Serikali ya Sudan. Ripoti ilionyesha kuna ukosefu wa kudhaminia kihakika haki za kimsingi kwa raia wakati wa kupiga kura, ikijumlisha uhuru wa kukusanyika, uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kusema, ikiwa miongoni mwa masuala kadha ambayo yameyafanya baadhi ya mashirika ya kiraia kutokuwa na imani kuhusu uchaguzi ujao. KM ameisihi Kamisheni ya Uchaguzi wa Taifa Sudan kuchukua hatua halisi zitakazohakikisha raia wote waliong\'olewa makazi pamoja na wahamiaji, na wale waliokosa vitambulisho, huwa wanajumuishwa kwenye miradi ya uchaguzi. KM alisema UM upo tayari kutekeleza mpango wa awamu mbili utakaotumiwa kuzisaidia kamisheni 25 za uchaguzi katika majimbo, kwa kusafirisha vifaa vye kuendesha uchaguzi kama inavyotakikana kisheria.

Kamati ya UM Kufidia Malipo ya Uvamizi wa Kuwait imeidhinisha Serikali ya Taifa la Kuwait ilipwe dola milioni 430 zitakazotumiwa kufadhilia wadai 10 waliopata hasara ya kimaisha kufuatia uvamizi wa 1990 wa majeshi ya Iraq katika Kuwait. Duru hii ya malipo inajumlisha dola bilioni 28 ya fidia kamili iliolipwa wadau husika tangu Kamati kuanza kazi zake. Fungu kubwa la fedha za malipo ya fidia hizi lilikusanywa kwa kuuza mafuta ya Iraq chini ya ule mradi uliokuwa ukijulikana kama ‘Mradi wa Chakula-kwa-Mafuta/Oil for Food Program', uliositisha shughuli zake mwaka 2003, kama ilivyoamrisha Baraza la Usalama. Kamati ya Kufidia Malipo ya Uvamizi wa Kuwait ilianzishwa rasmi 1991 kuwa ni chombo kisaidizi cha Baraza la Usalama cha kufanya mapitio ya maombi ya kulipwa fidia kutoka wadai karibu milioni 3, ikijumlisha maombi ya serikali 100, pamoja na maombi ya mashirika na raia binafsi.