Skip to main content

Ban anasema ni muhimu kwa Mataifa kuhitimisha mashauriano ya mkataba wa kudhibiti hali ya hewa

Ban anasema ni muhimu kwa Mataifa kuhitimisha mashauriano ya mkataba wa kudhibiti hali ya hewa

KM Ban Ki-moon leo alikuwa na mazungumzo ya kila mwezi na waandishi habari wa kimataifa waliopo hapa Makao Makuu ya UM. Kwenye taarifa ya ufunguzi KM alizingatia zaidi suala la athari za mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni na juhudi za kimataifa za kulidhibiti tatizo hili.

KM alisema anatarajia viongozi wa serikali na Mataifa 100 ziada, watakaohudhuria mkutano mkuu ujao kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, utakaofanyika Makao Makuu, mwezi Septemba - pale kikao cha 64 cha Baraza Kuu kitakapokutana - ya kwamba viongozi hawa watajitahidi "kufikia makubaliano" ya kuridhisha, kabla ya mwisho wa mwaka huu. Makubaliano haya yanafungamana na mkataba mpya wa kimataifa wa kudhibiti uchafuzi wa hewa, ambao utasailiwa mwezi Disemba watakapokusanyika wawakilishi wa kimataifa kukamilisha majadiliano yao kwenye mji wa Copenhagen, Denmark.