Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

KM ameshtushwa na mapambano ya kimadhehebu Nigeria Kaskazini

KM ameshtushwa na mapambano ya kimadhehebu Nigeria Kaskazini

Kadhalika, Ijumanne, KM alitoa taarifa maalumu yenye kuelezea wasiwasi wake mkuu juu ya ripoti za kuzuka, hivi majuzi, duru nyengine ya mapigano ya kimadhehebu katika Nigeria kaskazini, vurugu ambalo limesababisha korja ya vifo.

 Ofisi ya Msemaji wa KM iliripoti Ban Ki-moon "ameshtumu vikali vitendo hivi vilivyosababisha upotezaji wa maisha ya watu kihorera na uharibifu wa mali," vurugu lilioendelezwa na wale raia wa Nigeria wanaodaiwa kuwa na "misimamo mikali ya kisiasa." KM alitumai "wale walioendeleza vurugu hili watatambuliwa na kufikishwa mahakamani haraka, kwa kufuatana na sheria za Nigeria." Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari kuanzia Ijumapili iliopita inakadiriwa watu 100 waliuawa kutokana na mapigano hayo ya kimadhehebu baina ya makundi ya WaIslamu wenyeji na vikosi vya polisi. KM aliwatumia mkono wa taazia jamaa na aila zote za raia waliopoteza maisha pamoja na kuwaombea majeruhi wapone haraka kutokana na madhara ya fujo. Vile vile KM ameiomba Serikali ya Nigeria, pamoja na taasisi za usalama na zile za kutekeleza sheria nchini, ikijumlisha pia viongozi wa kidini na jamii zinazohasimiana, kujaribu kukabiliana kwa pamoja na vyanzo vya mapigano ya kidini yanayoibuka nchini mwao mara kwa mara. Mwelekeo huu, anaamini KM, utayawezesha makundi husika yote kufikia suluhu ya kudumu, kwa kupitia njia za mazungumzo yatakayowakilisha mafahamiano na hali ya kuvumiliana kitamaduni baina yao.