Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjumbe wa UM kwa Usomali asema msaada wa jumuia ya kimataifa unahitajika kidharura kurudisha utulivu nchini

Mjumbe wa UM kwa Usomali asema msaada wa jumuia ya kimataifa unahitajika kidharura kurudisha utulivu nchini

Baraza la Usalama lilikutana leo asubuhi kuzingatia hali katika Usomali. Risala ya ufunguzi ya Mjumbe Maalumu wa KM kwa Usomali, Ahmedou Oul-Abdallah iliwahimiza wajumbe wa Baraza kuchukua "hatua thabiti" zitakazosaidia kurudisha tena utulivu kwenye taifa hili la Pembe ya Afrika, hasa katika kipindi cha sasa ambapo mapigano ndio yameshtadi zaidi kati ya majeshi ya mgambo wapinzani ya Al-Shabaab na Hizb-al-Islam dhidi ya vikosi vya Serikali, uhasama ambao ulizuka tena upya mjini Mogadishu mnamo tarehe 07 Mei (2009).

Ould-Abdallah alieleza kwamba umma wa Usomali pamoja na viongozi wao wa kijadi, hawaungi mkono katu fujo wala vurugu, na hawakubaliani na msimamo wa wale wenye kuendeleza vurugu nchini mwao. Alisema licha ya kuwa makundi husika na uhasama yalitiliana sahihi maafikiano ya amani, na serikali mpya iliundwa pamoja na raisi mpya kuchaguliwa, hata hivyo mafanikio haya hayakuweza kuzuia mapigano kuzuka tena Usomali mnamo miezi ya karibuni. Wakati huo huo UM umethibitisha ya kuwa tangu mwanzo wa mwezi Mei watu 200,000 waliong'olewa tena makazi kwa sababu ya mapigano, na wingi wao walijikuta bila ya mastakimu ya kujisitiri kwa mara ya pili katika miezi ya karibuni.