'Juhudi ziada zahitajika kukomesha uhamisho wa mabavu Uganda Kaskazini', aonya mtetezi wa IDPs

17 Julai 2009

Walter Kaelin, Mjumbe Maalumu wa KM juu ya Haki za Kibinadamu kwa wahamiaji wa ndani ya nchi (IDPs) amenakiliwa akisema ameingiwa moyo na kufurahika kwa "maendeleo aliyoyashuhudia kuhusu utekelezaji wa mahitaji ya watu waliong\'olewa makazi, kwa sababu ya mapigano, katika Uganda Kaskazini, ambapo takriban asilimia 80 ya umma huo, unaojulimsha wahamiaji milioni 1.8, wamesharejea vijijini mwao kwa khiyari."

Aliyasema haya baada ya kumaliza ziara ya wiki moja katika Uganda. Alielezea shukrani zake kwa juhudi za Serikali ya Uganda za kuwapatia wahamiaji wa ndani fursa ya kutafuta suluhu ya kudumu juu ya masaibu yao, na aliyakaribisha pia mafanikio yaliopatikana katika kurejesha uhuru wa kutembea na usalama wa raia katika eneo la kaskazini, ambapo siku za nyuma eneo hili lilihanikiza vurugu na hali ya wasiwasi ilioendelezwa na waasi wa kundi la LRA. Juu ya yote hayo, Kaelin anaamini bado kuna vizingiti fulani vilivyoselelea dhidi ya juhudi za kudumisha utulivu na amani ya eneo - mathalan, alisema kuna fungu la wahamiaji wa ndani ambao hawaamini usalama umerejea kwenye vijiji vyao, na kwa mujibu wa kanuni za kimataifa hairuhusiwi kuwalazimisha wahamiaji hawa kurejea makwao bila ya idhini yao." Kwa hivyo, alisisitiza Mjumbe huyu wa KM, Serikali itawajibika ama kuwaunganisha wahamiaji hawa na jamii za eneo ziliopo kambi za mastakimu ya muda,au kuwatafutia makazi mengine nje ya eneo, kama ilivyoidhinishwa na sera ya Uganda juu ya wahamiaji wa ndani ya nchi (IDPs).

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter