Skip to main content

Waathirika wa uhasama katika JKK wafadhiliwa $7 milioni na Mfuko wa CERF kukidhi mahitaji ya kimsingi

Waathirika wa uhasama katika JKK wafadhiliwa $7 milioni na Mfuko wa CERF kukidhi mahitaji ya kimsingi

Taasisi ya Mfuko wa UM juu ya Maafa ya Dharura au Mfuko wa CERF imetangaza ya kuwa itafadhilia msaada wa dola milioni 7, kukidhi mahitaji ya dharura kwa watu 250,000 waliopo kwenye majimbo yenye matatizo ya Kivu Kusini na Kaskazini.

Kwa ushirikiano na wenye Serikali, mashirika ya UM yanayohudumia misaada ya kiutu yatawapatia familia husika mahitaji ya kimsingi, ikijumlisha makazi ya muda, maji safi na usafi wa mazingira na vile vile huduma ya afya ya msingi na ilimu, pamoja na kuwasaidia kihali wale wanawake walionusurika kutokana na karaha ya kunajisiwa kimabavu na udhalilishaji wa kijinsia. Ross Mountain, Mratibu wa UM juu ya Misaada ya Kiutu katika JKK alisema hii leo kutoka Kinshasa ya kwamba "kuongezeka kwa vitendo vya kutumia nguvu na fujo dhidi ya raia, vinavyoendelezwa na waasi wa kigeni walio wafuasi wa kundi la FDLR, wakichanganyika na baadhi ya askari wahuni wa jeshi la taifa, wamesababisha maelfu ya familia kung'olewa makazi, wingi wao wakiwa raia waliolazimika kuhama makazi mara kadha kabla ya hapo." Msaada wa dharura wa UM unatarajiwa kuwawezesha waathirika hawa kukidhi vyema mahitaji yao ya kimsingi.