Skip to main content

Hapa na pale

Hapa na pale

Upande wa mashtaka, kwenye kesi ya ya mshtakiwa Thomas Lubanga Dyilo, kiongozi wa jeshi la mgambo la JKK (Union of Congolese Patriots) katika jimbo la mashariki la Ituri umeripotiwa kukamilisha kuwasilisha ushahidi wake dhidi ya mtuhumiwa, mbele ya Mahakama ya Kimataifa juu ya Makosa ya Jinai ya Halaiki (ICC) iliopo Hague. Lubanga ni mtuhumiwa wa awali kuwekwa rumande chini ya uangalizi wa mahakama, na kesi yake inawashirikisha, kwa mara ya kwanza katika historia ya sheria ya kimataifa, waathirika wa mashitaka wakati kesi ikiendeshwa, ikijumlisha vile vile watoto wapiganaji. Lubango ameshtakiwa makosa mawili juu ya jinai ya vita: kuandikisha na kuwaunganisha watoto wapiganaji, chini ya umri wa sheria, kwenye jeshi la mgambo la kundi lake, fungu ambalo lilioshiriki kwenye mapigano nchini baina ya Septemba 2000 mpaka Agosti 2003. Mnamo kipindi cha wiki 22, watu 28 walitoa ushahidi - ikijumuisha wataalamu watatu - umma ambao vile vile walidadisiwa na kuhojiwa na mawakiliwanaomtetea mshitakiwa. Takriban mashahidi wote wa upande wa mashitaka walipatiwa ulinzi, pamoja na hifadhi iliowakinga na mashambulio, mathalan, sauti zao zilibadilishwa wakati walipotoa ushahidi na nyuso zao hazikuonyeshwa na walipewa hata majina ya bandia kuficha utambulizi binafsi. Waathirika karibu 100 walishiriki kwenye kesi tangu kuanza kusikilizwa mnamo tarehe 26 Januari (2009).

Joaquim Chissano, Mjumbe Maalumu wa KM kwa amani ya maeneo yalioharibiwa na mashambulio ya waasi wa kundi LRA katika Uganda Kaskazini, leo asubuhi aliwakilisha risala ya mwisho juu ya kazi zake mbele ya Baraza la Usalama, kabla ya kujiuzulu wadhifa aliodhaminiwa na KM mwezi Disemba 2006. Chissano alichanganua hali ya utekelezaji wa mpango wa amani wa Juba na athari za operesheni za kijeshi za vikosi vya Uganda - vikosi ambavyo katika miezi ya karibuni vilishirikiana na wanajeshi wa mataifa jirani - dhidi ya kundi la LRA, baada ya kiongozi wake, Joseph Kony, kushindwa kutia sahihi Maafikiano ya Mwisho ya Amani. Alipendekeza Chissano, kwa nchi jirani na Uganda, kushirikiana zaidi kukabili hatari inayozushwa na vitimbi vya wapiganaji wa LRA, ambao waligundulikana, mara nyingi, kuhujumu raia na kulipiza kisasi kwenye maeneo ya JKK na Sudan Kusini, kufuatia operesheni za vikosi vya Uganda vya kuwasaka na kuwatoa mafichoni wapiganaji wa LRA. Chissano aliwaambia wajumbe wa Baraza la Usalama maafikiano ya amani ni lazima yatekelezwe hata hali ikiwa vipi. Alikumbusha kwamba umma muathiriwa wa Uganda Kaskazini, kwa sasa, wanavuna faida ya utulivu na amani ya eneo lao kwa sasa, hali ambayo jamii ya kimataifa inawajibika kuimarisha. Kufuatia taarifa ya Mjumbe wa KM kwa Maeneo Yalioathirika na Mashambulio ya LRA, Raisi wa Baraza la Usalama kwa Julai, Balozi Ruhakana Rugunda wa Uganda alitoa taarifa ya Baraza kwa waandishi habari, iliompongeza Chissano kwa mchango wake; na kuisihi LRA kuchukua fursa iliowadia hivi sasa kwa kutia sahihi Maafikiano ya Mwisho ya Amani.

Kwenye mji wa Geneva, Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) limeanzisha rasmi siku ya leo, mradi maalumu, wa kuwahudumia watoto wadogo wanaokabiliwa na mazingira ya dharura. Mradi umetayarisha Vifaa vya Kusaidia Mafunzo ya Msingi ya Utotoni, vifaa ambavyo hupatiwa watoto wanaojikuta wamekabiliwa na matatizo ya dharura, mathalan, vita au maafa ya kimaumbile. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF, Ann Veneman, huduma hii ni ya aina ya pekee kuandaliwa na jamii ya wahudumia misaada ya kiutu ulimwenguni. Vifaa vimo kwenye aina ya kisanduku chenye vitu 37 tofauti, vilivyokusudiwa kutumiwa na watoto 50 wenye umri wa mpaka miaka sita. Miongoni mwa vitu viliomo kisandukuni ni pamoja na dhumna, penseli za rangi, vidude vya kuchezea watoto kujengea, na michezo ya kukumbuka, vifaa ambavyo vitawasaidia watoto wadogo kujihusisha na watu na kupata hisia ya kumiliki vitu baada ya kupoteza vitu vyao vya kujliwaza kimaisha kwa sababu ya mapigano au maafa ya kimaumbile.

Naibu KM Asha-Rose Migiro Ijumanne alihutubia kwenye Makao Makuu, lile Kundi Linalotetea Haki Sawa za Wanawake katika UM (GERWUN). Alikumbusha kwenye risala yake ya kuwa lengo la kuleta usawa wa kijinsiya katika shughuli za UM ni kadhia mojawapo muhimu inayofungamana na jitihadi hakika za kuwasilisha mageuzi ya kuridhisha kwenye taasisi hii ya kimataifa. Alisisitiza mweleko huo ukitekelezwa utaisaidia UM kuwa na watumishi wepesi kikazi, wenye uwezo na ujuzi tofauti na uwajibikaji kwenye majukumu wanaodhaminiwa nayo - wafanyakazi wataotambuliwa kuwa na ari ya kutekeleza maadili ya kiwango cha juu kabisa kwenye kazi zao. Alisema UM ni lazima siku zote uwe na makali ya kujiandaa kuleta mageuzi ya kitaasisi, inapohitajika, kwa kutenda wanayoyahubiri. Alikiri kwamba ni vigumu kwa mwanamke kusarifu wizani unaofaa kati ya shughuli za ajira na ulezi, hali ambayo inawakabili wafanyakazi wengi wa kike wa UM. Alisema kuna upungufu wa wanawake wenye vyeo vya juu katika baadhi ya idara muhimu za UM, kama zile idara zenye kuhusika na operesheni za ulinzi amani za UM, na kwenye vitengo vya UM vinavyoshughulikia masuala ya kisiasa, hali ambayo husababishwa na mila za kikale zenye kubagua wanawake.

Kamati ya UM Kuondosha Aina Zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW) ikijumuika na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) zimeandaa warsha maalumu wa siku mbili, utakaofanyika Makao Makuu kuanzia Alkhamisi hadi Ijumaa, ambapo kutasailiwa matatizo ya ubaguzi wa wanawake na matumizi ya mabavu ya kijinsia dhidi ya wanawake wahamiaji, hususan kwenye maeneo ya mapigano na uhasama. Wahamiaji waathirika kutokea mataifa ya Bhutan, Zimbabwe na Liberia wanatarajiwa kutoa ushahidi wao kwenye warsha, wakijumuika na wahamiaji wa ndani ya nchi kutokea Chechnya na Kenya, halkadhalika.

Wakati alipokuwa Sharm el-Sheikh kuhudhuria Mkutano wa Mataifa ya Umoja wa Mataifa Yasiofungamana na Mataifa Makuu (NAM), KM Ban Ki-moon vile vile alipata fursa ya kuhutubia, kwa mara ya awali, Mkutano wa Wake wa Viongozi kuhusu huduma za kusimamia udhibiti bora wa mizozo. Alisema kwenye risala yake "tunawajibika kuwaangalia wanawake,kwa mtazamo wa kuwa wao ndio  mawakala wa mageuzi", na mwelekeo huu, aliongeza kusema, ndio wenye kuongoza UM katika shughuli zake, ambapo haki za wanawake zinahishimiwa na kutetewa, na watumishi wa kike hujumuishwa kwenye harakati zote za kikazi. Alisema chini ya uongozi wake, kundi kubwa la wanawake aliwateua kuchukua vyeo kadha vya hadhi ya juu, uteuzi uliokiuka majira yaliopita, na uliongeza kwa mara tatu, idadi ya wafanyakazi wanawake wenye nyadhifa za juu za uongozi.