Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Ofisi ya Msemaji wa KM imeripoti kuwa Ban Ki-moon alishtushwa sana na kuhuzunishwa na taarifa alizopokea juu ya mauaji ya Zill-e-Usman, mtumishi raia wa Pakistan mwenye cheo cha juu katika Ofisi ya UM Juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR), mauaji yaliotukia kwenye kambi ya wahamiaji ya Katcha Garhi karibu na mji wa Peshawar, Pakistan. Usman alishambuliwa na watu waliojaribu kumteka nyara wakati alipokuwa anatoka kwenye kambi ya wahamiaji. Alipigwa risasi kifuani mara kadha na alifariki baadaye kutokana na majeraha aliopata kwenye tukio hili. Kadhalika, mlinzi wa kambi aliuawa kwenye shambulio, na mfanyakazi mmoja raia wa UM pamoja na mlinzi mwengine walijeruhiwa. KM amelaani vikali shambulio katili hili dhidi ya watumishi wa UM waliojitolea kusimamia misaada ya kiutu kwa umma muhitaji wa Pakistan. Licha ya tukio hili, UM umeripoti utaendelea kuhudumia mahitaji ya idadi kubwa ya waathirika wa maafa Pakistan na kuwanusuru maisha. KM aliwatumia aila zote za waathirika wa tukio hili pamoja na Serikali ya Pakistan mkono wa pole.

Baraza la Usalama lilikutana Alkhamisi asubuhi kuzingatia Sierra Leone. Kwenye risala alioiwakilisha Stephen Rapp, Mwendesha Mashtaka wa Mahakama Maalumu juu ya Jinai ya Vita katika Sierra Leone alieleza kwamba Mahakama yao inathaminiwa na raia wa Sierra Leone, na ni taasisi yenye umuhimu mkubwa kwa maelfu ya watu waliolemazwa kwa kukatwa viungo, na kwa makumi elfu ya watu waliouawa kihorera, pamoja na mamia elfu ya raia walionajisiwa na kujamiiwa kimabavu. Alizungumzia pia juu ya kesi inayoendelea hivi sasa kwenye mji wa Hague, Uholanzi ya aliyekuwa Raisi wa Liberia, Charles Taylor, uendeshaji mashtaka ambao alisisitiza unatekelezwa kwa utulivu, uangavu unaoridhisha wa hali ya juu, kwa haki na kwa ufanisi. Alibashiria hukumu ya kesi ya Taylor itatolewa mnamo kati ya 2010, na shughuli za kusikiliza rufaa zitakamilishwa mahakamani mwanzo wa 2011. Rapp alisema shughuli za kuendesha mashtaka zinazofanyika kwenye Mahakama Maalumu ya Jinai ya Vita Sierra ya Freetown, harakati hizi, alitilia mkazo, zimewasilisha maendeleo mapya ya kihistoria kuhusu kanuni za sheria ya kiutu ya kimataifa.

Jaji Renata Winter, Raisi wa Mahakama Maalumu juu ya Jinai ya Vita katika Sierra Leone naye pia alihutubia Baraza la Usalama ambapo aliwaambia wajumbe waliohudhuria mkusanyiko huo, ya kuwa Mahakama Maalumu yao ni ya awali kuhalalisha hukumu au uamuzi tangulizi juu ya makosa ya jinai dhidi ya utu kwa kuandikisha kimabavu na kuwatumia watoto wadogo chini ya umri wa sheria, kwenye mapigano, na vile vile kuharimisha kisheria mashambulio ya walinzi amani wa UM pamoja na ndoa za kulazimishwa. Kadhalika, Jaji Renata alisisitiza juu ya ulazima wa kukamilisha kesi ya Charles Taylor kwa sababu kesi hii ni "muhimu katika kuhakikisha hali ya utulivu na amani inayoregarega katika ukanda wa Afrika Magharibi itaendelezwa au la."

Ijumaa Baraza la Usalama litazingatia ripoti ya KM kuhusu operesheni za Shirika la UM Kutunza Amani Sudan Kusini (UNMIS). Alain Le Roy, Naibu KM wa UM juu ya Operesheni za Ulinzi Amani Duniani ataisailia ripoti, kwa kutathminia, awali, tatizo la kuongezeka kwa mapigano ya kikabila yenye kuhatarisha utulivu wa taifa zima, na kukosoa yale mapendekezo ya Mapatano ya Amani ya Jumla ya kuitisha uchaguzi na kura ya maoni miongoni mwa raia waliokuwa wakihasimiana kwa miongo kadha. KM alisema ndani ya ripoti kadhia za kurudisha utulivu unaosarifika zitategemea uhusiano wa karibu miongoni mwa makundi yote yaliopo katika nchi. Ripoti vile vile itazingatia ushirikiano wa Serikali ya Sudan, mashirika ya UM na wadau wenzi juu ya juhudi za kuhudumia umma, kufuatia uamuzi wa kufukuza nchini wafanyakazi wa mashirika yasio ya kiserikali yaliokuwa yakihudumia misaada ya kihali nchini mnamo tarehe 04 Machi (2009.

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti kwamba mashirika ya UM yaliopo Benin sasa yanajishughulisha kidharura kuwasaidia watu walionusurika maafa ya mafuriko yaliozuka kwenye taifa hilo la Afrika Magharibi baada ya mvua kali kunyesha katika wiki za karibuni. Kwa mfano, Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) linafadhilia msaada wa fedha zitakazotumiwa kuratibu mpango wa kutathminia namna ya kufarajia, kwa ufanisi, mahitaji ya umma. Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF), kwa upande wake, limefadhilia tembe 3,000 za klorini kusafishia uchafu wa kwenye maji, na vile vile imegawa vyandarua 1,000, pamoja na masaada wa dola 100,000 za kuhdumia shughuli za maji safi na usafi wa mazingira na katika kampeni za mafunzo ya afya bora. Wakati huo huo, Shirika la UNHCR juu ya wahamiaji limetoa msaada wa mablanketi, vyandarua, mikeka na mahema kwa waathirika wa mafuriko, wakati Shirika la UM juu ya Udhibiti wa Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) linajiandaa kufadhilia huduma bora za uzazi kwa watu husika.