Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Henry Anyidoho, Naibu Mjumbe Maalumu wa Pamoja wa UM-UA kwa Darfur (UNAMID), Ijumanne alizuru Darfur Magharibi na kukutana na wahamiaji waliorejea makwao vijijini katika siku za karibuni. Wakati huo huo, Tume ya Umoja wa Afrika kwa Darfur, inayoongozwa na Raisi mstaafu wa Afrika Kuisni, Thabo Mbeki, ikijumlisha vile vile waliokuwa viongozi wa mataifa yao - Pierre Buyoya wa Burundi na Abdulsalami Abubakar wa Nigeria - nao pia walizuru Darfur ya Kaskazini na kukutana na makamanda wa tawi liliojitenga la Abdul Wahid kutoka kundi la waasi la SML.

Mashirika 40 ya UM na yale yasiokuwa ya kiserikali yenye kuhudumia misaada ya kiutu, leo yametoa mwito wa pamoja, kutokea Jerusalem, unaoitaka serikali ya Israel kukomesha, halan, vikwazo vyote vilioekewa lile eneo liliokaliwa kimabavu la WaFalastina la Tarafa ya Ghaza, ambalo wiki hii linashuhudia mwaka wa pili wa vikwazo hivyo. Wakazi WaFalastina milioni 1.5 walilazimika kutegemea kufadhiliwa misaada ya kihali kutoka wahisani wa kimataifa ili kumudu na kunusuru maisha yao kwa sababu ya vikwazo. Taarifa hiyo ya pamoja vile vile ilibainisha kwamba jumla ya vitu na bidhaa zinazoruhusiwa kuingia Ghaza kwa sasa, kufuatia vikwazo vya Israel, ni sawa na robo moja tu ya ile idadi iliokuwa ikiingia Ghaza kukidhi mahitaji ya umma, kabla ya vikwazo hivyo kuwekwa. Mashirika yanayohudumia misaada ya kiutu yamehadharisha kwenye taarifa yao ya kuwa sera karaha ya kuukaba uchumi wa Ghaza imezusha ukosefu mkubwa wa ajira, ambao haujawahi kushuhudiwa hapo kabla, na kusababisha umaskini uliohanikiza na kufurutu ada, maafa yalioanzisha hali ya kutegemea, kikamilifu, kutoka wahisani wa kimataifa, ile misaada ya kumudu maisha. Kadhalika mwito wa pamoja wa mashirika, umeitaka Israel iyaruhusu fursa na uhuru kamili wa kuendeleza shughuli zao zote zinazohusikana na ugawaji wa misaada ya kiutu, kama ilivyoidhinishwa mikataba ya kimataifa, kwa kulingana na haki za binadamu zinazotambuliwa kote ulimwenguni, na kuambatana, halkadhalika, na viwango vya sheria hakika ya kimataifa. Taarifa ya makundi yanayohudumia misaada ya kiutu Ghaza vile vile imetaka wenye madaraka Israel kuruhusu biashara ya kawaida ifanyike kwenye eneo husika bila vizingiti na, hatimaye, kuwawezsha raia wa KiFalastina huko kujitegemea kimaisha, hali ambayo itapunguza ukosefu wa kazi na umaskini.

KM ameanzisha leo Tume ya Ushauri wa Kisomi juu ya Mabdiliko ya Hali ya Hewa na Nishati iliojumlisha viongozi wa kibiashara, wataalamu na wale wanaohusika na huduma za nishati, ambao anatumai watamsaidia kuchangisha, kwa wakati, sera za kuimarisha udhibiti bora wa masuala yanayohusu hali ya hewa na nishati. Wataalamu hawa wa Tume ya Ushauri watampatia KM nasaha za kitaaluma juu ya uhusiano wa mambo yalivyo kwenye majadiliano yanayohusu mabadiliko ya hali ya hewa, na kumsaidia kutambua masuala gani ya kuzingatiwa kwa kina, kabla ya kujumuika Mkutano Mkuu wa Copenhagen, hususan yale masuala yenye kufungamana na jukumu muhimu la ufanisi wa nishati, kukabili taathira za mabadiliko ya hali ya hewa. Tume ya Ushauri ilikutana leo Makao Makuu kwa mara ya kwanza kwa mashauriano, chini ya uongozi wa Kandeh Yumkella, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) na Mwenyekiti wa UM juu ya Masula ya Nishati.

Mashirika yanayohudumia misaada ya kiutu katika JKK yametoa ombi la dharura linalopendekeza kufadhiliwa msaada wa dola milioni 38, utakaotumiwa kuokoa maisha ya raia karibu milioni moja walioathirika na hali ya mtafaruku na usalama wa kigeugeu kwenye eneo la mashariki. Taarifa iliotolewa na Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeeleza kwamba mchango huo ukikamilishwa utatumiwa kuhudumia kihali watu 800,000, hasa watoto na wanawake, walioathirika na mashmbulio ya makundi yenye silaha pamoja na operesheni za kijeshi katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini. Wiki kadha za mapigano kwenye eneo hilo zilisababisha raia wengi kuishi katika shida kuu na hali ya kiutu dhaifu kabisa, ambayo ililazimisha halaiki ya umma kung'olewa makazi, na kusababisha pia mauaji yaliokithiri, na vitendo karaha vya kunajisi wanawake kimabavu vinavyoendelezwa na wapiganaji. Ross Mountain, Mratibu wa UM juu ya Misaada ya Kiutu katika JKK amethadharisha kwambamiezi ijayo itakuwa ya usumbufu mkubwa kwa maelfu ya watoto, umma wa kiume na wanawake nchini.