Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Ripoti mpya iliotolewa leo na UM inaeleza kwamba asilimia 30 ya vijana wa Afrika, kati ya umri wa miaka 17 mpaka 25, huogopa kutoa maoni au kujieleza hadharani. Kutokana na bayana hii, Shirika la UNICEF na washiriki wenzi wameamua kupanua zaidi, na kuimarisha ule ukurasa wa jukwaa lao la intaneti/wavuti, wenye mada isemayo "Zungumza kwa Uwazi Afrika", ulioandaliwa hasa kwa madhumuni ya kuwasaidia vijana wa Afrika kushiriki kwenye majadiliano yenye maana kuhusu masuala muhimu yanayoathiri bara lao.

Raisi mstaafu wa Marekani, Jimmy Carter, Ijumanne alisimamia taadhima maalumu za kutunukia zawadi wale wanafunzi waliopo kwenye eneo liliokaliwa la Tarafa ya Ghaza, waliofuzu daraja ya juu ya masomo yanayohusu haki za binadamu, yalioongozwa na Shirika la UM Linalofarajia WaFalastina wa Mashariki ya Karibu (UNRWA). Taasisi hii ya UM ilielezea shukrani zake kuu kwa Raisi Carter kushiriki kwenye taadhima zao, na UNRWA ilitangaza kujivunia pakubwa na mchango wake wa kuwapatia wanafunzi wa KiFalastina katika Ghaza mafunzo muhimu juu ya haki za binadamu.

Baraza Kuu la UM lilikutana asubuhi kwenye kikao maalumu kufanya mapitio juu ya maendeleo kwenye jitihadi za kimataifa za kukabiliana na matatizo ya UKIMWI ulimwenguni. Maofisa wa UM wa ngazi za juu, waliohutubia mkutanoni walizihimiza nchi wanachama kudumisha, na pia kuimarisha ahadi walizotoa siku za nyuma za kukabiliana na matatizo ya UKIMWI, katikati ya kipindi ambapo uchumi wa dunia unaendelea kuporomoka. Maofisa hawa walionya kwamba kupunguza misaada ya kuhudumia kadhia hiyo katika kipindi cha sasa, ni kitendo kitakachozusha gharama na mateso makubwa kwa umma katika siku zijazo. Raisi wa Baraza Kuu, Miguel D'Escoto alisema kwenye risala yake kwamba watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI (VVU) wamo hatarini sasa hivi, kwa sababu ya migogoro ya kifedha na uchumi inayolemaza na kuharibu uchumi wa dunia nzima, kwa ujumla. Kutokana na mazingira haya, aliongeza, serikali nyingi zilionekana kuanza kupunguza miradi ya kudhibiti UKIMWI na kuridhia hali hiyo kwa kukwepa majukumu yao. Aliwakumbusha wajumbe wa kimataifa kwamba hali inapokuwa ngumu ndipo imani halisi na maadili hakika ya ubinadamu wetu yanapobainika kidhahiri. KM Ban Ki-moon, aliwahadharisha wajumbe waliohudhuria mkutano wa Baraza Kuu, "kutotumia mzozo wa uchumi wa kimataifa kama ndio kisingizio cha kukatiza ahadi zao - na kuyahimiza mataifa kuitumia hali hiyo kuwa ni kichocheo cha kuwezeka vitega uchumi imara vitakavyowapatia vizazi vijavyo natija za afya kwa muda mrefu." Vile vile KM alitilia mkazo umuhimu wa kukomesha chuki, ubaguzi na fedheha kwa wale raia waliopatwa na VVU/UKIMWI - na alikumbusha kwamba thuluthi moja ya Mataifa Wanachama bado haijabuni sheria inayokataza ubaguzi dhidi ya wagonjwa wa virusi vya UKIMWI.

Ijumatatu Baraza la Usalama lilishindwa kupitisha azimio la kurefusha madaraka ya operesheni za Shirika la UM la Uangalizi wa Kusitisha Mapigano Georgia (UNOMIG) kwa sababu ya kura ya turufu/vito ya mjumbe wa kudumu wa Shirikisho la Urusi. Matifa kumi yalipiga kura ya upendeleo, kuongeza muda wa operesheni za UNOMIG katika Georgia, wakati nchi nne kutopiga kura. Kufuatia uamuzi huo KM amelazimika kumuamrisha Johan Verbeke, Mjumbe Maalumu anayeongoza shughuli za amani Georgia kuchukua hatua zote zinazohitajika kusitisha, halan, operesheni za UNOMIG, kuanzia siku ya leo.

KM alikutana Ijumanne na wawakilishi wa hadhi ya juu wa Cameroon na Nigeria wanaohudhuria Kamati ya Kufuatilia utekelezaji wa Maafikiano ya Greentree ya tarehe 12 Juni 2006, kuhusu suluhu ya mzozo wa mipaka baina ya mataifa mawili haya. Mkutano huu ni wa awali kati ya KM na wawakilishi wa vyeo vya juu wa Cameroon na Nigeria tangu mwafaka wa kuhamisha madaraka ya eneo la ugomvi na uhasama la Ghuba ya Bakassi, liliokabdhiwa rasmi Cameroon, mnamo tarehe 14 Agosti 2008.

Radhika Coomaraswamy, Mjumbe Maalumu juu ya Haki za Watoto Walionaswa kwenye Mapigano pamoja na UNICEF wametoa mwito wa kuchukuliwa hatua za haraka, za kuwahifadhi watoto wanaojikuta wamenaswa kwenye mazingira ya uhasama na mapigano. Mwito ulitolewa Ijumanne pale ilipowasilishwa ‘Ripoti ya Mapitio ya Miaka 10 ya Machel' kuhusu hali ya watoto kwenye maeneo ya vurugu na fujo. Graça Machel aliyeteuliwa na KM kama mtaalamu huru juu ya haki za watoto, aliwasilisha mbele ya Baraza Kuu ripoti yenye mada isemayo "Athari za Mapigano kwa Watoto". Ripoti hii iliihamasisha jumuiya ya kimataifa kuanzisha Ofisi ya Mjumbe Maalumu wa KM Kutetea Haki za Watoto Walionaswa kwenye Mapigano. Kwa mujibu wa ripoti ya mapitio, jumla ya watoto bilioni moja hivi sasa wanaishi katika mataifa au maeneo yalioathirika na mapigano - jumla hiyo ni sawa na sehemu moja kati ya sita ya idadi yote ya watu ulimwenguni. Ripoti ilihadharisha pia kwamba athari za mapigano dhidi ya watoto katika karne ya sasa ni za kikatili sana. Watoto hujeruhiwa na silaha ndogo ndogo zilizosambaa kwa wingi kimataifa, na pia huumizwa na kudhalilishwa na makundi haramu yenye kuchukua silaha, majeshi ya mgambo ambayo huwalazimisha watoto wa umri mdogo kushiriki kwenye mapigano. Kadhalika watoto hushambuliwa katika skuli na hospitali na kunajisiwa kimabavu. Ripoti inapendekeza mataifa yote wanachama yatekeleze haraka majukumu yao ya kuwapatia raia wadogo wa umri, hifadhi bora, kwa kuongeza zile juhudi za kubuni sheria mpya na kuandaa sera na hatua za utendaji zitakazonusuru watoto wadogo na madhila yanayotokana na mazingira ya mapigano.

Ripoti ya KM juu ya Guinea-Bissau iliotolewa leo, ilipitia shughuli za Ofisi ya UM ya Kujenga Amani nchini humo na pia kusailia maendeleo ya kisiasa ya karibuni. Miongoni mwa mapendekezo ya KM yaliojumuishwa kwenye ripoti ni pamoja na azimio linalowataka wenye madaraka kuzingatia hatua kadha za kukomesha duru za fujo na makosa ya kutenda jinai bila kukhofu adhabu, ikijumlisha rai ya kubuni bodi la uchunguzi juu ya matukio ya vurugu nchini. Kadhalika KM ameiomba jamii ya kimataifa kuipatia Guinea-Bissau msaada wa kusuluhisha, kwa amani, mgogoro wa nchini, na papo hapo kuwataka wazalendo kutimiza dhamana za kiraia wakati wakijitayarisha kushiriki kwenye uchaguzi wa raisi utakaofanyika mwezi ujao.

Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limetangaza kuchukizwa sana na mashambulio ya karibuni yaliofanyika Sudan Kusini dhidi ya matishali yaliobeba misaada ya chakula, tukio ambalo ilisema humaanisha hali huko inaendelea kuharibika na kuathiri umma unaotegemea misaada ya kihali ya UM. Ripoti za UM zinasema jumla kadha ya maofisa wa polisi wa Sudan walioshindikiza matishali hayo walishambuliwa na kuuawa na makundi ya kikabila, wapiganaji ambao baadhi yao pia waliuawa vile vile. Msafara wa vyombo 27 vilivyobeba tani 735 za msaada wa chakula ulikuwa unaelekea kwenye maeneo ambayo watu 19,000 waliong'olewa makazi walikuwa wakisubiri ruzuku hiyo. WFP inasema boti 11 zake zimepotea kutokana na mashambulio hayo, na inasisitiza tukio hili lilikuwa "pigo kubwa" dhidi ya kazi zake za kuhudumia misaada ya kiutu Sudan Kusini. Kwa sababu ya shambulio hilo WFP imetangaza sasa italazimika kutumia ndege kusafirisha misaada yake, hatua ambayo itaathiri sana kiwango cha chakula kinachopelekwa kwenye maeneo husika, kwa sababu ndege hazina uwezo mkubwa wa kubeba shehena ya chakula, zinaweza kuchukua tani tano kwa wakati mmoja.