Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Kikao cha 62 cha Baraza Kuu la Afya Duniani kilifunguliwa rasmi, Ijumatatu (18/05/2009) mjini Geneva, ambapo Mataifa Wanachama 193 wa Shirika la Afya Duniani (WHO) hukutana kila mwaka kujadilia masuala muhimu yanayohusu afya ya jamii, mathalan, namna ya kukabiliana kimataifa na miripuko hatari ya maambukizi ya janga la homa ya mafua; utekelezaji wa Sheria za Afya ya Kimataifa, pamoja na utunzaji wa afya ya msingi, ikijumlisha vile vile na ustawishaji wa mifumo ya afya, viukilio vya afya ya jamii, na nidhamu zinazohitajika kutekelezwa kufuatilia vyema mafanikio yanayohusu Maendeleo ya Malengo ya Milenia juu ya afya. Masuala ya bajeti pamoja na usimamizi wa shughuli za WHO nayo pia husailiwa mkutanoni.

Mnamo mwanzo wa wiki, KM Ban Ki-moon alimaliza ziara ya siku mbili katika Bahrain ambapo aliwasilisha Ripoti ya Dunia ya Makadirio ya Kupunguza Hatari ya Maafa. Kwenye risala yake KM aliwahimiza viongozi wa kimataifa kuwekeza zaidi kwenye huduma za kupunguza hatari inayotokana na maafa ya kimaumbile, mathalan, kwenye taaluma ya kubashiria mitetemeko ya ardhi na matofani. Alisema maafa kama haya hayazuiliki, lakini anaamini pakiwepo maandalizi ya kuridhisha kubashiria dharura kama hizi walimwengu angalau watadiriki kupunguza madhara yanayotokana na maafa kama haya ya kimaumbile.

Ujumbe wa Baraza la Usalama unaotembelea mataifa manne katika Afrika Ijumatatu uliwasili Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK) na walizuru kambi ya wahamiaji wa ndani ya nchi (IDPs) iliopo Kiwanja, karibu na mji wa Goma, katika jimbo la Kivu Kaskazini. Walipokuwepo huko walikutana na wawakilishi wa wahamiaji wa IDPs karibu 13,000 na kusikiliza matatizo wanayokabiliwa nayo kuhusu usalama wa raia. Walishauriana taratibu za kuimarisha ulinzi bora na usalama Kivu Kaskazini, kwa ushirikiano kati ya Serikali ya JKK na vikosi vya amani vya UM vya MONUC. Wajumbe wa Baraza la Usalama pia walifanya mapitio ya kufufua huduma za uchumi na maendeleo katika JKK. Kabla ya hapo ujumbe ulitembelea Kigali, Rwanda na kukitana na Raisi Paul Kagame. Walizungumzia masuala yanayohusu uimarishaji wa amani katika mashariki ya JKK na katika eneo la Maziwa Makuu. Kwenye mguu wa safari katika Ethiopia, Ijumamosi iliopita, wajumbe wa Baraza walikutana na Waziri Mkuu, Meles Zenawi kwa majadiliano juu ya hali katika Usomali na vile vile kusailia namna ya kukwamua mzoroto wa mpango wa amani kati ya Ethiopia na Eritrea. Ijumanne ujumbe utaelekea Kinshasa kwa mazungumzo ya kiwango cha juu na maofisa wa serikali, ikijumlisha Raisi Joseph Kabila wa JKK.

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura imeripoti mahitaji ya kiutu katika Usomali yanazidi kukithiri bila ya kiasi, kwa sababu ya kuendelea kwa mapigano, ikichanganyika na hali mbaya ya ukame nchini. Juu ya hali hiyo OCHA haikufanikiwa kupokea msaada wa dola milioni 984, mchango unaotakikana kukidhi mahitaji ya kiutu ya umma, na kwa sasa OCHA imepokea asilimia 37 tu ya lile Ombi la Mfuko wa Jumla. Kwa mujibu wa OCHA, raia 3.2 milioni - sawa na asilimia 40 ya idadi ya watu Usomali - watendelea kutegemea misaada ya kiutu kutoka wahisani na wafadhili wa kimataifa hadi Septemba 2009, ili kunusuru maisha.

Kwenye ufunguzi wa kikao cha 8 cha Tume ya Kudumu ya UM juu ya Masuala Yanayohusu Wenyeji wa Asili (UNPFII) Naibu KM Asha-Rose Migiro alisema kwenye risala yake kwamba mkusanyiko huo ulifanyika katika wakati muhimu sana ambapo ulimwengu umekabiliwa na sanjari ya mizozo na migogoro inayohitajia suluhu za dharura, kwa sababu wanaodhurika zaidi na kuathirika na matatizo haya ni jamii za kiasili za ulimwengu. Alikumbusha kwamba zaidi ya hilo, jamii hizi za kiasili bado zinaendelea kuteswa na kusumbuliwa na dhulma ya ubaguzi na dharau. Kwa hivyo, aliyahimiza Mataifa Wanachama kujitahidi kuharakisha utekelezaji wao wa yale mapendekezo ya Mwito wa Azimio liliopitishwa 2007 juu ya Haki za Wenyeji wa Asili duniani.