Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Taasisi ya Takwimu ya Shirika la UM juu ya Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) imeripoti kwamba kutokana na uchunguzi uliofanyika karibuni juu ya viwanda vya michezo ya sinema duniani imebainika wazi kwamba Nollywood, yaani kiwanda cha kutengeneza filamu cha Nigeria, kinakaribia kuziba pengo la kadhia hiyo na Bollywood, kiwanda cha kutengeneza filamu za sinema katika Bara Hindi.

Robert Serry, Mratibu Maalumu wa UM juu ya Mpango wa Amani kwa Mashariki ya Kati Ijumanne alikutana mjini Cairo, kwa mazungumzo, na Waziri wa Nchi za Kigeni wa Misri Ahmed Aboul Gheith pamoja na Waziri wa Ulinzi na Usalama Omar Suleiman na vile vile KM wa Umoja wa Nchi za Kiarabu, Amr Moussa. Kwenye mazungumzo yao walizingatia na kusailia hali katika eneo la WaFalastina la Tarafa ya Ghaza, pamoja na kujadilia juhudi za upatanishi za makundi yanayohasimiana ya KiFalastina, na kuzingatia shughuli za walowezi wa Kiisraili kwenye eneo liliokaliwa la Magharibi ya Mto Jordan, na pia kubadilishana mawazo juu ya matumaini ya kurudia tena zile juhudi za kuleta suluhu itakayosaidia kuwa na Mataifa Mawili [ya Falastina na Israel] katika Mashariki ya Kati, juhudi ambazo zitakuwa za kuaminika na zilizo za kweli, na sio za kigeugeu. Serry alisema "walimwengu wanaamini kwamba wakati umewadia wa kuhakikisha kunapatikana mageuzi yanayoridhisha yenye uwezo wa kuhamasisha makundi husika kupatana, utaratibu utakaokomesha ukaliaji wa kimabavu wa ardhi zilizotekwa za WaFalastina na kuhitimisha, moja kwa moja, ugomvi wa muda mrefu katika eneo." Aliashiria Sery kwamba wiki zijazo zitakuwa ni muhimu kupima kama mazungumzo ya amani yanaonyesha dalili za kuendelea mbele na yatasarifika au yatakwenda kombo na kuzorota kwenye mazingira ya kigeugeu, sawa na hali ilivyo hivi sasa.