Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mawaziri wa Afya wakubaliana Beijing kuharakisha udhibiti bora wa TB sugu

Mawaziri wa Afya wakubaliana Beijing kuharakisha udhibiti bora wa TB sugu

Mkutano wa siku tatu, ulioandaliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Umma wa Uchina pamoja na Taasisi za Bill na Melinda Gates, ulifanyika Beijing wiki hii, kwa makusudio ya kushauriana juu ya mradi mpya wa utendaji, utakaofaa kutekelezwa kipamoja ili kudhibiti bora maradhi ya kifua kikuu, hususan kwenye yale mataifa yanayosumbuliwa zaidi na ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa fafanuzi za Shirika la Afya Duniani (WHO), wataalamu wamekadiria watu nusu milioni ziada huambukizwa, kila mwaka, na hii TB ya M/XDR, na hunyimwa uwezo wa kupata matibabu ya kuridhisha, hali ambayo hupalilia zaidi usumbufu wa kifua kikuu. Aina hii ya TB sugu huzusha msiba mkubwa kwa wagonjwa, familia na jamii zao, hali kadhalika. Vile vile kutokana na aibu za kimila dhidi ya waathirika wa maradhi huzusha hali ambayo huwaumiza wagonjwa, kimwili na kiakili. Aidha, WHO imeeleza gharama za kupima na kutibu TB ya M/XDR kwa mafanikio ni kubwa sana, na wagonjwa wanaoambukizwa maradhi hayo katika nchi masikini hawana uwezo wa kumudu jukumu hilo hata kidogo. Tishio hili la maradhi ya kifua kikuu linaweza kukomeshwa kimataifa, haraka, pindi mataifa husika yote yatashirikiana na wahisani wa kimataifa, kukabiliana, kwa nguvu moja, na janga hili la afya kwakulidhibiti mapema kabla halijafumka na kuhatarisha afya ya ulimwengu, kwa ujumla.

Shirika la WHO limeripoti hivi sasa ni nchi 50 wanachama zinazosumbuliwa kihakika na tatizo la TB ya aina ya M/XDR. Dktr Margaret Chan, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, kwenye risala alioiwakilisha mbele ya kikao cha 61 cha Baraza la Afya Duniani, aliuhadharisha ulimwengu kwamba pindi "TB ya M/XDR itaruhusiwa kuenea na kusambaa kimataifa, bila ya kudhibitiwa haraka na walimwengu, kuna hatari ya kuzusha janga la msiba mkuu ambao madhara yake yatakuwa ya kihistoria."