Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulimwengu sasa umo kwenye mkumbo wa awali wa maambukizo ya janga la homa ya A(H1N1), yahadharisha WHO

Ulimwengu sasa umo kwenye mkumbo wa awali wa maambukizo ya janga la homa ya A(H1N1), yahadharisha WHO

Shirika la Afya Duniani (WHO) wiki hii limepandisha kiwango cha tahadhari ya maambukizi ya homa ya mafua ya aina ya A(H1N1) kutoka daraja ya 5 mpaka ya sita.

Mnamo Alkhamisi ya tarehe 11 Juni (2009), Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dktr Margaret Chan, aliwasilisha mbele ya waandishi habari mjini Geneva, Uswiss, tangazo maalumu juu ya hali ya maambukizi ya homa ya mafua ya H1N1 kwa sasa katika dunia, kufuatia kikao cha kamati ya dharura ya taasisi hiyo ya afya, kilichowakusanyisha wataalamu kadha wa afya kuzingatia suala hilo. Dktr Chan alisema kiwango cha maambukizi ya homa ya mafua ya H1N1 kwa hivi sasa, yamefikia kiwango, kilicholazimika kutambuliwa rasmi kuwa ni janga la ugonjwa wa kuenea kimataifa. Hii ni mara ya kwanza, baada ya miaka 40, Shirika la WHO kutoa ilani kama hii juu ya tahadhari ya afya ya jamii ya kimataifa. Dktr Chan alielezea, kama ifuatavyo, sababu zilizoihamasisha WHO kutoa uamuzi huo:.

"Kwa kigezo cha ushahidi uliokusanywa sasa hivi, na uchanganuzi wa wataalamu wa kimataifa, kuhusu virusi vya homa ya mafua, kwa ujumla, tunaweza kuthibitisha kihakika kwamba ulimwengu sasa umetomea kwenye mkondo wa mazingira yaliovamiwa na janga la kuenea kimataifa kwa ugonjwa wa A(H1N1). Kwa hivyo, kuambatana na ushahidi huo wa kisayansi, nimeamua rasmi kupandisha juu kipimo cha tahadhari ya maambukizi ya homa ya H1N1, kutoka kiwango cha 5 hadi kiwango cha 6. Hivi sasa ulimwengu umeingia kwenye mkondo wa 2009 uliovamiwa na janga la ugonjwa wa homa ya mafua ya H1N1."

Kufuatia taarifa hiyo ya Mkurugenzi Mkuu wa WHO, KM Ban Ki-moon naye pia alizungumzia juu ya tatizo la kuenea kwa kasi kwa maambukizi ya homa ya mafua ya H1N1, kwenye mkutano wa kila mwezi aliokuwa nao hapo jana adhuhuri na waandishi habari waliopo Makao Makuu ya UM mjini New York. KM aliisihi jumuiya ya kimataifa kutoingiwa na kihoro kisio msingi, wala kujipatisha wasiwasi wa bure kwa sababu Shirika la Afya Duniani (WHO) limepandisha juu kiwango cha tahadhari ya maambukizi ya virusi vipya vya homa ya mafua ya A(H1N1), kutoka daraja ya 5 hadi 6. Alisisitiza kwamba kwa kulingana na hali inavyojulikana kitaaluma, kitu cha kutia maanani kwa sasa ni kuhakikisha walimwengu wote hujitayarisha, kwa ushirikiano wa pamoja, kukabiliana na mripuko wa maambukizi ya maradhi haya kitaifa na kimataifa, pindi tukio hili litafurutu ada. Alisema hatua zilizochukuliwa na WHO sasa hivi, kupandisha juu daraja ya maambukizo, ni kitendo ambacho humaanisha "imethibitishwa rasmi na wataalamu husika juu ya kuenea, kijiografia kwa ugonjwa", na ilani hiyo, haimaanishi katu "uchochezi wa khofu au wasiwasi wa kumahanisha umma wa kimataifa." Alikumbusha kwamba licha ya kuwa homa ya mafua ya H1N1 ni ugonjwa wa kuambukiza, virusi vyake havikuonyesha ukali wa kudhuru wanadamu kwa kiwango cha kuhatarisha maisha ya halaiki, kama ilivyokhofiwa hapo mwanzo maradhi yalipogunduliwa. Kima cha vifo vilivyosababishwa na virusi vipya vya H1N1, alitilia mkazo, ni kidogo. Hata hivyo, KM aliihimiza jamii ya kimataifa kutopwelewa na kuendelea kuwa "waangalifu", kwa sababu hakuna ajuaye ni mfumo wa aina gani maradhi haya yatakuja nayo mnamo miezi ijayo. KM alieleza virusi vya homa ya H1N1, kwa sasa, vimesambaa zaidi kwenye nchi zilizoendelea .. na hali hii inabashiriwa huenda ikabadilika haraka - na kuzusha taathira zisiojulikana kimataifa. Kwa mujibu wa takwimu rasmi za UM, mnamo saa 07:00 za majira ya GMT, Ijumaa ya tarehe 12 Juni (2009) watu "29,669 katika nchi 74 walisajiliwa kuambukizwa na ugonjwa homa ya mafua ya H1N1, ikijumlisha pia vifo 145."

WHO imeripoti kwamba hulka ya janga la ugonjwa unaoambukiza kimataifa huambatana na kasi ya maambukizo katika sehemu zote za dunia. Katika karne zilizopita, maambukizi ya maradhi kama ya homa ya mafua ya H1N1, yalikuwa yakichukua kati ya miezi sita mpaka tisa, juu ya kuwa usafiri wa kipindi hicho ulikuwa ukitegemea zaidi reli au meli. Usafiri wa karne ya sasa, unaotumia ndege, ndio wenye uwezo wa kueneza, kwa kasi zaidi, virusi vya maradhi ya kuambukiza kimataifa.