Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Maafisa wa idara ya huduma za dharura ya UM wamepongeza ushirikiano wa maafisa wa serekali ya Sudan katika kutathmini mahitaji ya huduma za dharura katika jimbo lenye ghasia la Darfur, wakati huo huo wakionya juu ya hatari zilizopo kufuatia kufukuzwa makundi muhimu ya misaada.

Zaidi ya wakimbizi 100 kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati walivuka mpaka wenye ghasia na kuingia kusini mashariki ya Chad mwishoni mwa wiki, wakiungana na zaidi ya wengine 6 800 waloanza kuingia mapema mwaka huu. Kufuatana na msemaji wa UNHCR Ron Redmond wakimbizi hao wepya wengi wao wanawake watoto na wazee, wameliambia shirika hilo kwamba wamekimbia mapambano kati ya vikosi vya serekali na waasi huko kaskazini ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la UM , UNHCR linaeleza kwamba kuzorota kwa hali ya usalama katika baadhi ya sehemu za Kusini mwa Sudan, kunazuia kurudi kwa wakimbizi kutoka Uganda, Kenya na Ethiopia. Wiki iliyopita, malalamiko ya ghasia yaliyopangwa kwa pamoja na wapiganaji wa zamani kutoka kundi la SPLA, walokua wanadai malipo na marupurupu yao ya miezi mitano, yalizuia kazi katika baadhi ya miji ya majimbo ya Kati na Mashariki ya Equatoria na kuvuruga maisha kwa siku kadhaa.