Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Hapa na Pale

Msemaji wa KM Ban Ki-moon, baada ya mkutano na waandshi habari Ijumatano adhuhuri, ameripoti KM kukaribisha kuapishwa kwa Morgan Tsvangirai kuwa Waziri Mkuu mpya wa Zimbabwe. Alisema kitendo hicho kilimaanisha hatua muhimu imechukuliwa na Zimbabwe, katika kutekeleza Mapatano ya Amani ya Septemba 15 (2008). Serikali mpya ya muungano wa taifa Zimbabwe ilinasihiwa kuikabili mizozo ya kiuchumi na kiutu yaliolivaa taifa, haraka iwezekanavyo, ikijumlisha tatizo sugu la mripuko wa maradhi ya kipindupindu ambayo yanaendelea kusumbua umma katika Zimbabwe.

Ripoti mpya ya KM kuhusu operesheni za vikosi vya mchanganyiko vya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kwa Darfur (UNAMID), iliowasilishwa kwenye Baraza la Usalama, imehadharisha kwamba ongezeko la vurugu katika Darfur ni hali inayoashiria makundi yanayohusika na mzozo wa eneo wamepania kuwezeka zaidi kwenye mapigano, badala ya kujishirikisha kwenye majadiliano ya kurudisha amani, kama walivyoahidi hapo kabla.  KM alishtumu vurugu liliofunika Darfur na athari zake kwa raia. Alirudia tena kwenye ripoti, lawama zake dhidi ya kundi la waasi wa JEM, kwa kushambulia eneo la Muhajeriya, na pia ameilaumu Serikali ya Sudan kwa mashambulio ya ndege za kijeshi katika eneo hilo hilo la Darfur. Ripoti ya KM ilikumbusha kwamba vikosi vya UNAMID havitoweza kuendeleza operesheni zao kama walivyodhaminiwa na Baraza la Usalama mpaka pale watakapopatiwa helikopta zaidi. Alipendekeza kwa yale Mataifa Wanachama yenye uwezo wa kufadhilia vifaa na zana zinazohitajika na vikosi vya UNAMID kutekeleza majukumu yao katika Darfur, wafanye hivyo kidharura.

Baada ya mkutano wa hadhi ya juu kumalizika mjini Nairobi, kuhusu Mzozo wa Eneo la Pembe ya Afrika, UM umeripoti kwamba unakadiria watu milioni 20 wataendelea kuhitaji misaada ya dharura kieneo ili kunusuru maisha. UM unasema mataifa yalioathirika sana kimaumbile ni yale ya Ethiopia, Usomali, Kenya, Uganda na Djibouti. Imeripotiwa kwamba ijapokuwa katika miezi ya Oktoba na Disemba kulinyesha mvua za kawaida katika maeneo husika, hata hivyo hali ya chakula haionyeshi dalili ya kutengenea kwa sababu kadha, ikijumlisha tatizo la kufumka kwa bei za chakula, kutanda kwa vurugu, usalama uliopwelewa na kutokana na kusambaratika kwa shughuli katika soko la kimataifa. UM unakadiria dola bilioni mbili zitahitajika katika 2009 kukidhi mahitaji ya chakula ya umma wa maeneo husika.