Skip to main content

Hapa na pale

Hapa na pale

Hapa na Pale

Mji wa Copenhagen umesajiliwa Alkhamisi kuwa mshiriki wa 100 wa ushirikiano unaojulikana kwa umaarufu kama Mtandao wa Mazingira ya Hali ya Hewa Huru, ambao huongozwa na Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP). Mwaka mmoja uliopita Mtandao wa Mazingira ya Hali ya Hewa Huru ulianzishwa rasmi kimataifa, kwa madhumuni halisi ya kukuza shughuli maalumu zitakazohakikisha umma wa kimataifa utaishi kwenye jamii zenye uchumi usiosumbuliwa na mazingira yaliopambwa na hewa chafu.

Karen Abu Zayd, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika Linalofarajia Wahamiaji wa KiFalastina wa Mashariki ya Karibu (UNRWA) alikutana na wabunge watatu wa Marekani waliozuru Alkhamisi eneo liliokaliwa la Tarafa ya Ghaza. Abu Zayd alionana kwa mazungumzo na Seneta John Kerry, aliye Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti juu ya Masuala ya Nchi za Kigeni. Kadhalika, alikutana na wabunge wawakilishi, Brian Baird na Keith Ellison ambao walichukua fursa ya kuyazuru Makao Makuu ya UNRWA na pia zile sehemu za Ghaza zilizoharibiwa na kuangamizwa na mashambulio ya karibuni ya Israel. Wabunge hawa wa Marekani walipatiwa fafanuzi kamili kuhusu hali ya kiutu ilivyo Ghaza hivi sasa, na ripoti juu ya shughuli za UNRWA pamoja na taarifa kuhusu matatizo yanayosababishwa na ukosefu wa ruhusa ya kuingiza bidhaa Ghaza, kwa kupitia vivuko vya mipaka na Israel.

 Shirika la UM Linalosimamia Ulinzi wa Amani katika JKK (MONUC) limeripoti ya kuwa Ijumamosi litaanzisha mafunzo maalumu kuhusu kanuni za mahakama za kijeshi, kwa watumishi wa jeshi la taifa 580, wakijumlisha makamnda wa vitani, wanasheria, pamoja na wasajili na watumishi wa ofisi ya mwendesha mashtaka, mainspekta wa polisi na vile vile wale makarani wa mahakama. Mafunzo haya yataendelezwa mpaka mwisho wa mwezi Juni, katika sehemu mbalimbali za JKK. Masomo yatafanya mapitio ya madftari ya sheria ya JKK na vile vile kusailia sheria za kiutu za kimataifa, na kuchanganua, halkadhalika, namna ya kukabiliana na makosa ya kijinsiya dhidi ya kuingilia watu kimabavu, na mafunzo juu ya utaratibu wa usimamizi wa mahakama za kijeshi, na maadili na kanuni za kikazi kwa maofisa wa mahakama.  Lengo halisi la mradi huu ni kuimarisha uwezo wa kikazi kwa wale waliodhaminiwa majukumu ya kutekeleza sheria ya kijeshi nchini Kongo.

Mkutano wa siku tatu juu ya shughuli za uchukuzi wa baharini, uliotayarishwa na Shirika la UM juu ya Biashara na Maendeleo (UNCTAD), umekamilisha majadiliano mjini Geneva na kutoa mwito maalumu, wenye kupendekeza viwanda kukuza juhudi zao katika kupunguza umwagaji wa hewa chafu angani. Kwa mujibu wa taarifa ya mkutanoni, shughuli za usafiri wa baharini nazo pia hujumuisha asilimia nne ya hewa chafu inayomwagwa angani katika dunia, na inakhofiwa kama tatizo hili halijadhibitiwa mapema jumla hiyo inaashiriwa itaongezeka mara tatu ya kiwango cha sasa itakapotimu 2050. Wataalamu mkutanoni walipendekeza miundo ya vyombo vya baharini irekibishwe iweze kudhibiti bora matatizo hayo, na vile vile walitaka marekibisho yafanyike kwenye injini za meli na katika matumizi yao ya nishati.

Kwenye kikao kilichoandaliwa Beijing, kwa sehemu, na Shirikala UM la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani (WMO) majadiliano yalilenga kwenye taratibu za kukabiliana, kwa mafanikio, na ukame mkali ulionekana kuzuka mara kwa mara duniani katika miaka ya karibuni, janga ambalo huchanganyika na hali mbaya ya hewa iliyokiuka mipaka. Baadhi ya wataalamu mkutanoni walithibitisha kuwepo matatizo haya kwa kutoa mfano wa kufumka karibuni  kwa hali mbaya ya joto, ukame haribifu na moto wa kasi kuu katika taifa la Australia.