Skip to main content

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Mjumbe Maalumu wa KM kwa Usomali, Ahmedou Ould Abdallah amekaribisha uamuzi wa kiongozi wa upinzani, Sheikh Sharif Sheikh Ahmed kurejea Mogadishu karibuni baada ya kuhajiri mji kwa muda wa miaka miwili mfululizo. Kwa mujibu wa Ould Abdallah, kurejea kwa Sheikh Ahmed kwenye mji mkuu, kunaashiria matarajio ya kutia moyo, hasa kwenye zile juhudi za kurudisha utulivu na amani nchini kwao. Mwezi Juni 2008, Sheikh Ahmed aliongoza Umoja wa Makundi ya Ukombozi wa Pili wa Usomali, ambao wafuasi wake waliridhia, pamoja na Serikali ya Mpito yale Mapatano ya Djibouti ya kusitisha uhasama na mapigano. Maafikiano haya vile vile yalipendekeza UM upeleke vikosi vya kimataifa kulinda amani na kurudisha utulivu Usomali, eneo la Pembe ya Afrika ambalo tangu 1991 halijajaaliwa kuwa na serikali ya taifa.

Baraza la Usalama limekutana Ijumatano asubuhi, kwa mashauriano, kuzingatia hadhi ya Vikosi vya Uangalizi wa Kusimamisha Mapigano katika Milima ya Jolan (UNDOF), kufuatia mazungumzo na wawakilishi wa nchi zilizochangisha wanajeshi wazalendo, kwa niaba ya UM, kutumiwa kuimarisha usalama katika eneo hilo la Syria. Madaraka ya vikosi vya UNDOF, yaliodahaminiwa na Baraza la Usalama kuendeleza operesheni zake, yanatarajiwa kumalizika mwisho wa mwezi Disemba.

Shirika la UM la Kufarajia Wahamiaji wa KiFalastina wa Mashariki ya Karibu (UNRWA) limeripoti limefanikiwa kupokea malori 13, Ijumatano ya leo, yalioruhusiwa kuingia Ghaza na shehena za mafuta ya kupikia pamoja na madawa, shehena ambazo UNRWA imeripoti na kusisitiza haziridhishi kamwe kukidhi mahitaji ya jumla ya umma unaoishi kwenye eneo liliozingiwa la Tarafa ya Ghaza. Wakati huo huo, Naibu Kamishna Mkuu wa UNRWA, Filippo Grandi, kwenye mkusanyiko wa kikao cha kuchangisha misaada ya kimataifa kwa bajeti la UNRWA la 2009, kilichofanyika Makao Makuu, alionya kwamba bila ya kurekibisha haraka mzozo wa fedha uliokabili shirika lao, UNRWA italazimika kupunguza huduma muhimu za kueleimisha na kusmamia afya ya jamii kwa umma wa KiFalastina. Mnamo mwanzo wa 2006 UNRWA iliweza kuchangisha akiba ya msaada, taslimu, wa dola milioni 60 uliofadhiliwa na wahisani wa kimataifa, akiba ambayo hivi sasa imeporomoka na kufikia dola milioni 1 tu katika Disemba 2008.

Benki Kuu ya Dunia imechapisha ripoti mpya inayozingatia Matarajio ya Uchumi wa Kimataifa kwa 2009. Ripoti inasema utafiti wa Benki Kuu umethibitisha kuwepo mzoroto mkubwa wa shughuli za uchumi, takriban katika nchi zote za dunia, ikijumlisha pia yale mataifa yanayoendelea ambayo, kwa muda, uchumi wao ulikuwa, na kuongezeka, kwa kima cha kutia moyo. Jumla ya Pato la Mwaka la Dunia (GDP) linatabiriwa kuteremka mwaka huu, kutoka asilimia 2.9 hadi asilimia 0.9 katika 2009, hali ambayo itazifanya nchi tajiri kushuhudia ukuaji hasi wa uchumi. Vile vile ripoti inatabiri shughuli za biashara ulimwenguni, katika mwaka ujao, zitanywea na kupungua, kijumla, kwa asilimia mbili ziada, hali ambayo imeonekana kufufuka, kwa mara ya kwanza, kwenye soko la kimataifa baada ya robo karne. Wakati huo huo Benki Kuu ya Dunia imetangaza kuanzisha akiba ya dola bilioni 2, itakayotumiwa kuharakisha misaada na mikopo ya ushuru mdogo, kwa yale mataifa masikini sana ili kuyawezesha kumudu mizozo ya fedha iliopamba duniani katika kipindi cha karibuni.