Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Ijumanne (14/10/08) Shirika la UM juu ya Huduma za Ulinzi wa Amani katika JKK (MONUC) limeripoti kuanzishwa kwa kamati maalumu itakayosaidia kurahisisha utekelezaji wa maafikiano ya kujiondoa katika mapigano, miongoni mwa makundi yanayohasimiana, kwenye eneo la Kivu Kaskazini. Wajumbe waliohudhuria tafrija ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo itakayojulikana kama Kamati ya Muda ya Kushauri Operesheni za Kusitisha Mapigano Kivu Kaskazini, yenye wajumbe 20, ilijumlisha wawakilishi wa UM, Umoja wa Ulaya na wawakilishi wa serikali, pamoja na wafuasi wa baadhi ya majeshi ya mgambo ya eneo.

Tarehe 15 Oktoba inaadhimishwa pia kwa mara ya kwanza kuwa ni Siku Kuu ya Kimataifa kwa Wanawake wa Vijijini. Risala ya UM kuihishimu siku hii imekumbusha wanawake wa vijijini ndio wenye jukumu la kuzalisha zaidi ya nusu ya chakula kinachovunwa duniani na huchangia pakubwa katika kuzisaidia jamii zao kiuchumi. Lakini juu ya mchango wao unaonusuru maisha ya halaiki ya watu, wanawake hawathaminiwi wala hawalipwi fidia wanayostahiki.

Jacques Diouf, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) amehadharisha Serikali za kimataifa kutopunguza misaada ya maendeleo ya kilimo katika nchi maskini au kuanza kutekelza zile sera za kulinda viwanda vya kizalendo kwa sababu ya matatizo ya fedha kwenye sokola kimataifa.

Raisi wa Baraza Kuu la UM, Miguel D’Escoto kwenye taarifa aliowasilisha mbele ya mjadala wa wawakilishi wote, kuzingatia mchango wa kimataifa unaotakikana kuimarisha Ushirikiano Mpya kwa Maendeleo katika Afrika (NEPAD) aliyakumbusha Mataifa Wanachama ahadi walizotoa kabla za kukidhi mahitaji ya maendeleo katika bara hilo, licha ya kuwa nchi zenye maendeleo ya viwandani nazo zinakabiliwa na mzoroto wa kiuchumi kwa hivi sasa.

Shirikisho la Ligi ya Malipo ya Mpira wa Miguu Ulaya, yenye kuwakilisha ligi 28 mbalimbali katika eneo hilo, imetangaza mjini Roma, Utaliana hii leo kuanzisha kampeni ya pamoja kupambana na tatizo la njaa ulimwenguni.