Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Alkhamisi (23 Oktoba) KM Ban Ki-moon atakutana na wataalamu wa watano wa uchumi, wa madaraka ya juu kimataifa, kwa makusudio ya kutathminia taathira za fedha kwenye kazi za UM duniani, na kulenga zaidi mashauriano yao kwenye juhudi za kutekeleza Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) na kukabiliana na taathira za mabadiliko ya hali ya hewa. KM alieleza, kwa kupitia msemaji wake, kwamba ni lazima kwa walimwengu kujumuika kwa moyo wa ushirikiano kukabiliana, kwa mafanaikio, na tatizo sugu la fedha kwenye soko la kimataifa, hasa ilivyokuwa mgogoro huu huumiza zaidi umma dhaifu na maskini.~

Msemaji wa KM, Michele Montas, kwenye mkutano na waandishi habari waliopo Makao Makuu, alikana madai yalioshtumu kwamba mashirika ya ulinzi amani ya UM Sudan yameipatia Mahakama ya Kimataifa juu ya Jinai ya Halaiki (ICC) taarifa za siri juu ya Darfur. Alieleza ya kwamba operesheni za ulinzi amani za UM katika Sudan hazikuendeleza upelelezi, wala hazijakusanya taarifa za siri za aina yoyote kwa niaba ya Mahakama ya ICC. Alitilia mkazo kwamba mashirika ya ulinzi amani Sudan yanawajibika kisheria kulipatia Baraza la Usalama ripoti ya jumla kuhusu shughuli zao, taarifa ambazo baadaye zinaweza kukabidhiwa Mahakama ya ICC pindi itapeleka maombi ya kupatiwa nyaraka hizo. Msingi wa ushirikiano baina ya Umoja wa Mataifa na Mahakama ya ICC umewekwa kwenye Mapatano ya Uhusiano yaliopitishwa kwa kauli moja mnamo 2004 kwenye Azimio 58/318 la Baraza Kuu. Kuhusu hali katika Darfur, Azimio 1593 (2005) la Baraza la Usalama limeshurtisha mashirika ya kiserikali na kikanda, pamoja na mataifa yote kushirikiana kikamilifu na Mahakama ya ICC. Ushirikiano huo unalingana kabisa na Azimio la Baraza Kuu, azimio la Baraza la Usalama Mapatano ya Uhusiano.

Shirika la UM juu ya Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limetangaza leo kuwa litachapisha ramani ya kwanza ya dunia yenye kuonyesha maeneo ya majabali na miamba inayotunza na kupitisha maji safi na salama chini ya ardhi (aquifers), sehemu zinazojumlisha asilimia 96 ya akiba ya maji katika ulimwengu. Ramani hii itawasilishwa wiki ijayo kwenye mtandao wa UNESCO, sawia na uwasilishaji wa mswada wa Mkataba wa Miamba ya Akiba ya Maji Iliovuka Mipaka. Ramani ya UNESCO itaonyesha zile sehemu za akiba ya maji zinazounganisha mipaka ya mataifa angalau mawili. Ramani hiyo itabainisha hadhi ya maji yanayaopatikana kwenye sehemu hizo na makadirio ya ujazaji tena wa akiba ya maji katika maeneo 273 yanayofunganisha mipaka – sehemu 68 hukutikana katika bara la Marekani, 38 katika Afrika, 65 kwenye Ulaya ya Mashariki, 90 katika Ulaya Magharibi na 12 kwenye bara la Asia.