Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

'Diplomasiya ndio yenye suluhu ya mgogoro wa JKK' - anasihi Doss

'Diplomasiya ndio yenye suluhu ya mgogoro wa JKK' - anasihi Doss

Alan Doss, Mjumbe Maalumu wa KM na Mkuu wa Shirika la UM juu ya Ulinzi wa Amani katika JKK (MONUC) amesema vikosi vya UM, kwa kufuatana na madaraka waliodhaminiwa na Baraza la Usalama, vinaendelea kuvisaidia vikosi vya taifa vya FARDC kulinda raia wa jimbo la Goma, umma ambao umejikuta kunaswa kwenye mapigano makali baina ya vikosi vya serikali na waasi wa kundi la CNDP, walio wafuasi wa Jenerali Mtoro Laurent Nkunda.

UM umepokea taarifa ziada mchana wa leo zenye kuonyesha hali katika Goma, na pia katika maeneo jirani, ni yawasiwasi mkubwa. Imeripotiwa ijapokuwa sasa hivi hakuna mapigano katika mji wa Goma, hata hivyo milio ya risasi bado inasikikana mara kwa mara kutokea maeneo yaliozunguka Goma. Wakati huo huo, Ofisi ya Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) imeelezea “mawimbi ya wanadamu” wahamiaji wa ndani, wanaokadiriwa 45,000 kutokea kambi ya Kibati, iliopo kilomita 10, walionekana wakifululizia Goma, kwa haraka na kwa khofu kubwa, kutafuta hifadhi, baada ya kushuhudia vikosi vya serikali vikiwakimbia wapiganaji waasi. Kuhusu wale wahamiaji wengine wa ndani 30,000 – ambao waliwasili kwenye eneo la Kibati hapo jana – nao walionekana kukimbia, mara ya pili tena, baada ya kusikia uvumi ya kwamba mapigano makali kati ya vikosi vya serikali na waasi wafuasi wa Laurent Nkunda, yameanza kujongelea maeneo yao. Mji wa Goma umemahanika kwa machafuko kamili kwa sasa hivi.

Taarifa nyengine inayoambatana na tukio hilo inasema UM umeripoti kwamba katika saa 24 zilizopita, wanavijiji 1,000 kutokea JKK waliripotiwa wamevuka mipaka na kuelekea taifa jirani la Uganda, na mamia ziada wengine wanaashiriwa, baadaye, nao pia wataelekea Uganda kunusuru maisha, kufuatia mapigano yaliofufuka kwenye eneo lao.

Shirika la Miradi ya Chakula (WFP) limetangaza ya kuwa litasubiri na kungojea mpaka hali itakapotulia katika Kivu, kabla hawajaanza tena huduma za kupeleka chakula kwa wahamiaji wa ndani. Hatua hii imechukuliwa kwa sababu ya ukosefu wa usalama katika eneo la mashariki. WFP hivi sasa imeshatayarisha malori 15 yenye shehena za chakula. Kwa makadirio ya UM tani 10,000 za chakula zinatakikana kila mwezi kuhudumia wahamiaji wa ndani waliopo Kivu. Ilivyokuwa idadi ya watu imeongezeka bila ya matarajio katika kipindi cha karibuni WFP itahitajia kufadhiliwa haraka misaada ziada ya chakula, na wahisani wa kimataifa, kuweza kumudu vizuri zaidi shughuli zao kama inavyostahiki, hasa ilivyokuwa wamebakiza akiba ya tani 4,000 tu za chakula kwa hivi sasa.