Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Majengo ya Umoja wa Mataifa yashambuliwa Usomali

Majengo ya Umoja wa Mataifa yashambuliwa Usomali

UM imethibisha hivi sasa ya kuwa majengo ya Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP), yaliopo kwenye mji wa Hargeysa, Usomali kaskazini leo asubuhi yalihujumiwa, mnamo milango ya saa nne, na kusababisha vifo na majeruhi kadha.

KM Ban Ki-moon amelaumu, kwa kauli nzito kabisa, mashambulio yaliotukia Ijumatano katika Usomali kaskazini, ikijumlisha pia lile shambulio la kujitolea mhanga liliofanyika kwenye majengo ya UNDP yaliopo Hargeysa, ambalo imeripotiwa gari liliokuwa na viripuzi lilitumiwa na kuua watumishi wawili wa UM, na kuumiza wafanyakazi sita wengine, na wawili kati yao inasemekana waliumizwa vibaya sana. KM alilaani vitendo hivi vya kutumia mabavu na fujo vilivyolenga, kwa makusudi, raia wa Usomali wasio hatia pamoja na kulenga watumishi wa UM ambao walikuwa wakienedelza kazi zao, bila uchofu, kwa lengo la kuwapunguzia mzigo wa maafa ya kimaisha raia wa Usomali walioathiriwa na vurugu na hali duni.