Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahojiano na M.Shirika, mwaathiriwa wa kunajisiwa kimabavu JKK

Mahojiano na M.Shirika, mwaathiriwa wa kunajisiwa kimabavu JKK

Mnamo mwezi Septemba Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF), kwa ushirikiano na wanaharakati wa Marekani wanaogombania haki za wanawake wa jumuiya isiyo ya kiserikali inayoitwa V-Day, walitayarisha warsha maalumu katika majimbo ya Bukavu na Goma katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK) ziliopewa mada isemayo “Wanawake Wavunja Ukimya na Miko ya Kijadi” – tukio ambalo, kwa mara ya kwanza, kihistoria, wale wanawake walionusurika na ajali ovu ya kunajisiwa kimabavu, walipata fursa ya kuelezea mateso yao hayo hadharani. Kitendo hiki kilitaka ujasiri mkubwa, na lengo hasa lilikuwa ni kuwasaidia waathiriwa kuyapunga yale marohani yaliowasumbua kiakili ili waweze kupiga hatua ya kusonga mbele kimaisha.

Mwandishi habari wa Redio ya UM, Jean-Pierre Ramazani alipata fursa ya kuwahoji, kwa njia ya simu, baadhi ya waathiriwa wawili walioshiriki kwenye warsha zilizoandaliwa bia na UNICEF na Jumuiya ya V-Day. Yafuatayo ni mahojiano na Mariamu Shirika ambaye anatumia lahaja ya Kiswahili cha Kikongo.