Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mukhtasari wa siku ya pili ya majadiliano ya jumla katika Baraza Kuu

Mukhtasari wa siku ya pili ya majadiliano ya jumla katika Baraza Kuu

Waziri Mkuu wa Uchina Wen Jiabao aliwaambia wajumbe waliohudhuria kikao cha wawakilishi wote cha Baraza Kuu kwamba sera adhimu ya taifa lake ni kufuatilia njia ya amani kukuza maendeleo,wakati ikijenga nguvu za kijeshi kwa makusudio pekee ya kulinda na kuhami uhuru wake na umoja wa nchi. Alisema Uchina hauna dhamira yeyote ya “kumiliki dunia, si sasa wala si katika siku zijazo.” Alifahamisha kwamba nchi yake haitishii taifa lolote, na kusisitiza Uchina inajivunia pakubwa kwa mafanikio yake katika ustawi wa kiuchumi, kuendeleza haki ya jamii, upole wa raia zake na uadilifu wenye nguvu.~

Raisi Shimon Peres wa Israel alisema kwenye hotuba yake,katika majadiliano ya Baraza Kuu,ya kuwa yeye binafsi anaamini mwelekeo wa mazungumzo ya hivi sasa kati yao na WaFalastina, yanaweza kukamilishwa katika kipindi cha mwaka mmoja, na kumalizika kwa kuwasilisha Mataifa mawili jirani ambayo raia zao wataishi kwa amani, usalama na katika hali ya kuhishimiana.

Raisi wa Senegal Abdoulaye Wade kwenye risala yake mbele ya kikao cha wawaklilishi wote alipendekeza wahisani wa kimataifa waekeze kwenye kilimo katika nchi zinazoendelea na kutumia utaratibu huo kukuza maendeleo badala ya kufadhilia misaada ya chakula, marekibisho ambayo, alitilia mkazo, yanahitajika kukabiliana na matatizo ya karne tuliomo hivi sasa. Alinasihi kwamba hatuwezi tena kutumia suluhu ya karne ya 20 kutatua matatizo magumu na ya pande nyingi ya karne ya 21 yanayoyakabili mataifa maskini.