Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kumbukumbu ya mkutano wa kimataifa juu ya UKIMWI - MEXICO

Kumbukumbu ya mkutano wa kimataifa juu ya UKIMWI - MEXICO

Raisi Mstaafu wa Botswana, Festus Mogae - ambaye anasifika kwa mchango wake mkubwa katika kupiga vita janga la UKIMWI nchini kwao - ameanzisha jumuiya mpya ya kundi la watu mashuhuri watakaomsaidia kukabiliana na janga la UKIMWI katika bara zima la Afrika. Kundi hili litajumuisha viongozi maarufu katika Afrika ambao watasaidia kuhamasisha umma barani humo kukuza juhudi za kudhibiti bora tatizo la kuenea kwa UKIMWI kwenye maeneo yao.

Wajumbe wa "Kundi la Watetezi dhidi ya virusi vya UKIMWI kwa Vizazi Huru" wanatazamiwa kuandaa sera madhubuti pamoja na hatua kadha za kufuatiliwa, kimataifa, ili kukomesha na kufyeka milele tatizo la kuenea kwa virusi vya UKIMWI katika Afrika. Miongoni mwa mapendekezo yatakayotiliwa mkazo zaidi na miradi hiyo ni pamoja na ile rai yenye kuwataka vijana wacheleweshe kushiriki kwenye vitendo vya kujamiana, na pia kupendekeza vijana wanaume watahiriwe. Baadhi ya wadau wengine wa kimataifa walioahidi kushirikiana na "Kundi la Watetezi kwa Vizazi Huru na Virusi vya UKIMWI" ni pamoja na BenkiKuu ya Dunia, Jumuiya ya UNAIDS, Shirika la Afya Duniani (WHO), Wakf wa Bill na Melinda Gates na pia Jumuiya ya Mfuko wa Kimataifa Kupiga Vita UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (the Global Fund).