Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Ijumamosi asubuhi KM alikutana ofisini kwake na timu maalumu ya washauri wakuu waliokusanyika Makao Makuu kujadilia namna UM inavyotakikana kukabiliana, kwa mafanikio, na hali ya mzozo uliozuka Georgia katika siku za karibuni.

Kadhalika, katika mwisho wa wiki KM alikuwa na mazungumzo na Mabalozi wanaowakilisha Wajumbe wa Kudumu wa katika Baraza la Usalama na kuonana, vile vile, na Mwakilishi wa Kudumu wa Georgia katika UM juu ya suala hili. Ofisi ya Msemaji wa KM iliripoti hali ya kiutu Georgia bado ni ya kutia wasiwasi na misaada ya kunusuru maisha katika maeneo ya magharibi haikuweza kufikishwa huko kwa magari na ililazimika kutumiwe ndege kwa sababu ya ukosefu wa usalama. Ijumapili misafara ya magari ya UM ilifanikiwa kuingia mji wa Gori, kwa mara ya kwanza, baada ya wiki mbili tangu vurugu kufumka kieneo. Hivi sasa mashirika ya WFP na UNHCR yamepeleka Georgia misaada ya biskuti maalumu za kuimarisha lishe kwa raia waathiriwa pamoja na kuwapatia madumu, vifaa vya jikoni na mablangeti. Hadi Ijumapili watu karibu 68,000 waliweza kufadhiliwa misaada ya kiutu na UM katika Georgia. Kadhalika, UM pamoja na mashirika wenzi yanayoshughulikia huduma za kiutu, yameanzisha kampeni ya kutaka ifadhiliwe mchango wa dola milioni 58.6 za kutumiwa katika miezi sita ijayo, kukidhi mahitaji ya watu 130,000 walioathirika na mzozo wa Georgia uliofumka majuzi, hususan wale waliong’olewa makwao na waathiriwa engineo wa mgogoro huo wa Ossetia Kusini.