Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

KM Ban Ki-moon alipohutubia Chuo Kikuu cha Taifa cha Seoul, katika Jamhuri ya Korea, baada ya kupokea shahada ya hishima, alitoa mwito maalumu kwa wananchi wenzake uliowataka waongeze mchango wao kwenye juhudi za kutatua masuala magumu yanayosumbua ulimwengu wetu, mathalan, kupanda kwa kasi kwa bei za chakula, mifumko ya bei za mafuta na vile vile hatari inayopaliliwa na ugaidi.

Jacques Diouf, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) alitoa nasaha maalumu mbele ya wabunge wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels, ambapo alisisitiza juu ya umuhimu wa kuharakisha michango yao katika kupiga vita njaa kwenye mataifa maskini. Alikumbusha kwamba mifumko ya bei za chakula katika 2007 ilisababisha athari mbaya ya njaa kwa watu milioni 50 katika mataifa yanayoendelea na sehemu nyengine za dunia.

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limetangaza kwamba limelazimika kupanua misaada ya chakula kwa Ethiopia, kwa sababu watu milioni 5 wanaokabiliwa na tatizo la njaa maututi wanahitajia kufadhiliwa haraka misaada hiyo kuwanusuru na vifo.

Ripoti ya KM juu ya hali ya utulivu katika Mataifa ya Afrika Magharibi imebainisha ya kuwa wingi wa nchi hizo, hivi sasa, zimefanikiwa kupitia kwa usalama kipindi cha mabadiliko, yaani kutokea mazingira ya vurugu na mapigano na kuelekea kwenye juhudi za kuimarisha amani, hali ambayo ni dhaifu, na inahitaji udhibiti bora kutoka mashirika ya kimataifa, chini ya uongozi wa UM. Lakini kuweza kuyakamilisha majukumu hayo kama inavyostahiki, ripoti ilitilia mkazo, UM na mashirika yake yatahitajia kufadhiliwa misaada maridhawa na wahisani wa kimataifa, mapema iwezekanavyo, kabla hali haijateleza tena kwenye vurugu na fujo.