Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM yaahidi kuisaidia Myanmar kukabiliana na athari za Kimbunga Nargisi

UM yaahidi kuisaidia Myanmar kukabiliana na athari za Kimbunga Nargisi

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imetangaza kuwa imeshatuma timu maalumu ya wataalamu wanaohusika na udhibiti wa maafa katika Myanmar, kufanya tathmini juu ya hasara na uharibifu ulioletwa na Kimbunga Nargis, kilichopiga nchini humo Ijumaa, tarehe 02 Mei, kimbunga chenye makali ya upepo ulirikodiwa kuvuma kwa mwendo wa kilomita 190 kwa saa. Maelfu ya watu inaripotiwa walifariki na mamia elfu wengine ama wamepotea au kujeruhiwa.

KM wa UM Ban Ki-moon, kwa upande wake, ametoa taarifa, kwa kupitia msemaji wake, iliobainisha yeye kuhuzunishwa sana na vifo vya watu na uharibifu uliojiri Myanmar katika mwisho wa wiki. KM aliwatumia salamu za pole ahli na aila zote za watu waliouawa, pamoja na wale waliojeruhiwa na kung’olewa makwao na Kimbunga Nargis. Hivi sasa timu ya huduma za dharura ya OCHA imejiandaa kuisaidia Serikali ya Myanmar kwa kila njia kuhudumia bora mahitaji yao ya kiutu kwa umma muathiriwa, pindi patihatajika msaada huu wa kimataifa.