Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huduma za mashirika ya UM katika Myanmar zasonga mbele

Huduma za mashirika ya UM katika Myanmar zasonga mbele

Elizabeth Byrs, Msemaji wa Ofisi ya UM juu ya Huduma za Dharura (OCHA) ameripoti kutoka Geneva kwamba hivi sasa juhudi za ugawaji wa misaada ya kiutu kwa waathiriwa wa Kimbunga Nargis zimefanikiwa kuwafikia watu milioni moja katika Myanmar, wingi wao wakiwa wakaazi wa mji mkuu wa Yangon. Kadhalika, aliripoti ya kuwa watu 470,000 nao pia walipatiwa huduma za dharura na mashirika ya kimataifa, ikiwa miongoni mwa watu milioni 2 muhitaji wanaoishi kwenye miji 15 iliopata madhara makubwa ya Kimbunga Nargis.

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) limearifu kwamba mamia ya watoto, waliokusanywa na ambao wazee wao hawajulikani walipo, nao pia watahitajiia kufadhiliwa haraka misaada ya kihali na jamii ya kimataifa kunusuru maisha.

Shirika la Kimataifa juu ya Wahamaji (IOM) limepeleka motaboti nne za aina ya Zodiac, zinazojazwa upepo, na kuendeshwa kwa kutumia injini, ambazo zitapelekwa katika eneo la Delta ya Irrawaddy, kusini ya Myanmar, kuhudumia afya wale raia waliong’olewa makwao, ambao sasa wamekusanyika kwenye makazi ya muda katika mahekalu na vituo vya faraja ya tufani, viliopo sehemu kadha za miji. Sehemu ya Delta ni vigumu kufikiwa na magari, na ni eneo lenye uharibifu mkubwa zaidi wa miundombinu kutokana na Kimbunga na Nargis.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kwamba bado halijapokea taarifa yeyote yenye kudai kuzuka kwa maambukizo ya maradhi Myanmar, kutokana na ajali ya tufani. WHO imesisitiza kuwa itaendelea kufuatilia, kwa karibuzaidi, hali ya afya nchini, kwa ujumla ili kuhakikisha kunakuwepo udhibiti bora wa siha za umma, ambao utahitajia kupatiwa huduma kinga za dharura dhidi ya maambukizo.