Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

KM anayaomba Mataifa Wanachama kuunga mkono mageuzi katika UM

KM anayaomba Mataifa Wanachama kuunga mkono mageuzi katika UM

KM Ban Ki-moon leo asubuhi aliwasilisha risala muhimu kwenye mjadala maalumu wa Baraza Kuu kuzingatia uwezekano wa kuleta mageuzi bora kwenye usimamizi wa kazi na shughuli za UM, sio katika Makao Makuu pekee bali vile vile kwenye mashirika yake kadha wa kadha yaliozagaa katika sehemu mbalimbali za dunia.

Kwenye risala yake mkutanoni KM alitoa mwito ulioyataka Mataifa Wanachama kuunga mkono mapendekezo aliowakilisha karibuni ya kutaka shughuli za UM ziimarishwe zaidi, hususan katika matumizi ya kukidhi mahitaji ya taasisi za UM, na katika ajira ya watumishi wenye maarifa na taaluma zinazohitajika kikazi, kwenye mazingira yatakayokuwa na uwazi mkubwa.

KM alisisitiza kwamba njia pekee itakayoiwezesha UM "kufuata mwelekeo wa kisasa, na kuendelea kuhudumia maadili mema ya UM ulimwenguni ni kuhakikisha tunawakilisha mfumo wa kisasa, unaokubali marekibisho yanayolingana na wakati, yalio madhubuti." Au kwa kauli nyengine, aliongeza kusema KM ni kuwa na UM "unaosimamiwa na kuongozwa vizuri zaidi kikazi."