Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi za UM kurudisha amani Kenya

Juhudi za UM kurudisha amani Kenya

Baraza la Usalama lilikutana Ijumatano jioni kushauriana juu ya udhibiti bora wa athari za machafuko yaliotukia Kenya hivi karibuni.

Baraza la Usalama limemwomba Katibu Mkuu kuripoti baadaye juu ya hatua za kuchukuliwa na Umoja wa Mataifa kuimarisha juhudi za upatanishi Kenya, na athari zake kwenye eneo na mataifa jirani. Kadhalika Baraza lilimtaka KM Ban aelezee taathira za machafuko Kenya dhidi ya operesheni za misaada ya kiutu nchini humo.

Mukhtasari wa matukio mengine katika Kenya:

Umoja wa Mataifa umearifiwa kwamba hali ya usalama nchini, sasa hivi, kwa ujumla, ni shwari lakini bado inatia wasiwasi.

Mazungumzo ya upatanishi kati ya Serikali na Chama cha Upinzani, yanayoongozwa na KM Mstaafu Kofi Annan yameripotiwa kuendelea kwa mwelekeo wa kutia moyo, hasa baada ya kujumuisha Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Kenya, mjumbe wa upinzani pamoja na Raisi Mstaafu wa Tanzania na Graca Machel wa Afrika ya Kusini.

John Holmes, Mshauri wa KM juu ya Misaada ya Dharura atawasili Kenya Ijumaa kwa ziara ya siku tatu ambapo atatathminia mahitaji ya kihali kwa umma ulioathirika na machafuko yaliyofumka nchini baada ya uchaguzi wa Disemba 2007.