Skip to main content

Hali ya utulivu yarejea Kenya

Hali ya utulivu yarejea Kenya

Inayofuata ni mukhtasari wa ripoti kuhusu shughuli za UM nchini Kenya ikiwa miongoni mwa harakati za kurudisha utulivu na amani kwa umma kijumla baada ya machafuko ya karibuni.

Mshauri wa KM juu ya Masula ya Kiutu, John Holmes, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) amewasili Kenya Ijumaa kwa ziara ya siku tatu kutathminia hali halisi ilivyo na kushauriana na wenye madaraka pamoja na mashirika ya UM juu ya hatua za kuchukuliwa kudhibiti bora huduma za kiutu nchini humo.

Ofisi ya OCHA imetangaza kwamba mashirika ya UM yataongeza huduma zake za ugawaji wa misaada ya kihali hususan maji safi pamoja na chakula na madawa.

Ijumanne Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeripoti huduma za ugawaji wa chakula zinaendelea vizuri kwenye zile kambi za wahamiaji wa IDPs, na malori yanayohusika na shughuli hizi yanapatiwa ulinzi wa wanajeshi wanapopeleka misaada hiyo kwenye sehemu za magharibi ya Nairobi.

Kadhalika, WFP imeripoti uandikishaji wa wanafunzi katika zile skuli zinazosaidiwa chakula, hususan katika mitaa ya mabanda iliopo karibu na jiji la Nairobi, imeteremka, kwa sasa, kwa kiwango cha asilimia 28, tangu machafuko yalipozuka katika nchi mwezi Disemba (2007).

Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya (KRCS) limetangaza takwimu zenye kuthibitisha ya kuwa kuanzia tarehe 5 Februari, jumla ya wahamiaji wa ndani ya nchi (IDPs), waliosajiliwa kuathirika na machafuko ya baada ya uchaguzi, imefikia watu 325,775 - umma huu hivi sasa umepatiwa makazi ya muda katika kambi 296 zilizotawanyika sehemu kadha wa kadha za nchi, na wahamiaji hawa hutegemea kufadhiliwa mahitaji ya kimsingi na mashirika ya kitaifa na kimataifa.

UM umearifiwa ya kuwa lile eneo la Kenya linalohusika na uzalishaji mkubwa wa chakula, hasa katika Bonde la Ufa/Rift Valley ni sehemu iliodhurika sana kwenye shughuli zake, kwa sababu ya machafuko ya karibuni.