Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM yasaidia Kenya kurudisha amani baada ya machafuko ya uchaguzi

UM yasaidia Kenya kurudisha amani baada ya machafuko ya uchaguzi

Timu inayowakilisha mashirika ya UM yanayohusika na miradi ya chakula duniani, WFP, maendeleo ya watoto, UNICEF na pia huduma za wahamiaji, UNHCR, ikijumuika na Jumuiya ya Kikatoliki juu ya Misaada ya Kiutu (CRS), Jumuiya ya Msalaba Mwekundu Kenya (KRCS) na mashirika mengine yasio ya kiserekali, yaani Shirika la World Vision International (WVI) na kundi la Kikatoliki la kufarijia maafa, Mercy Corps, yanashirikiana hivi sasa kipamoja kutathminia vizuri zaidi mahitaji ya kimsingi kwa umma uliopo eneo la Bonde la Ufa/Rift Valley, ambapo inaripotiwa ugawaji wa misaada ya kiutu unaendelea kwa usalama kama ilivyopangwa na idadi ya wahamiaji wa ndani ya nchi (IDPs) waliopo huko imetulia, na haijabadilika sana.~

Mnamo mwisho wa wiki iliopita, duru ya kwanza ya ugawaji chakula ilikamilishwa katika eneo la Bonde la Ufa Kusini.

Jumuiya ya Masalaba Mwekundu Kenya (KRCS) pamoja na Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) yanashirikiana kufanya makadirio ya pamoja juu ya mahitaji ya kimsingi katika wilaya zote ziliopo Jimbo la Kati.

Kadhalika, ripoti za UM kutokea Nairobi zimebainisha ya kuwa Bandari ya Mombasa hivi sasa inasimamia uangalizi wa makontena karibu 11,700 ikijumuisha makontena 500 ziada ya WFP. Huduma za usafirishaji wa bidhaa kutokea bandari hiyo zinaanza kuongezeka polepole na kurejea kiwango cha kawaida; mathalan, iliripotiwa kwamba katika mwisho wa wiki jumla ya tani za metriki 2,500 ziada za chakula zilipakiwa kwenye malori 84 na kupelekwa sehemu mbalimbali za Kenya na katika mataifa jirani.

Sehemu ya mwisho ya ripoti inakamilisha mahojiano ya simu tuliyofanya mapema wiki hii na Pamela Sittoni, Afisa wa Habari wa Ofisi ya Nairobi ya Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo ya Watoto (UNICEF) ambapo anajadilia huduma za ugawaji wa misaada ya kihali nchini pamoja na kuelezea hali ilivyo kwenye uandikishaji wa wanafunzi waliopo skuli za msingi na sekandari, baada ya utulivu kurejea taifani mwao.

Sikiliza mtandao kwa taarifa kamili.