Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huduma za UM kwa umma muhitaji Kenya

Huduma za UM kwa umma muhitaji Kenya

Mshauri Mkuu wa KM juu ya Masuala ya Kiutu, John Holmes, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) Ijumapili alikamilisha ziara ya siku tatu katika Kenya, ambapo alipata fursa ya kufanya makadirio ya binafsi kuhusu mahitaji hakika ya waathiriwa wa mzozo uliofumka nchini humo baada ya uchaguzi.~~

Holmes alikutana na waandishi habari mjini Nairobi ambapo alisisitiza kwenye risala yake juu ya kutopwelewa kwa UM katika juhudi za kuwapatia raia wa Kenya misaada ya kiutu, hususan wale wahamiaji wa ndani ya nchi (IDPs) kufuatia mabishano juu ya matokeo ya uchaguzi.

Alisema kwamba alipotembelea kambi za IDPs alikutana na wahamiaji mbalimbali ambao anaamini wingi wao walidhuriwa, sio kihali tu, bali vile vile “kiakili”. Alisisitiza juu ya wajibu wa taasisi ya kimataifa kufanya kila iwezalo, kuhakikisha umma huu unapatiwa mahitaji yao ya kihali, na pia matibabu ya kiakili, haraka iwezekanavyo.

Kadhalika Mshauri wa KM juu ya Misaada ya Dharura alitilia mkazo kwenye fafanuzi zake, ya kwamba UM itaendelea kuunga mkono juhudi zote za upatanishi, za kutafuta suluhu ya kuridhisha na UM utaaendelea kuhudumia misaada ya kiutu, kwa kila raia muhitaji, bila kujali uhusiano wa kisiasa wala kikabila.

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) kwa kulingana na takwimu zilizobainishwa mwisho wa wiki iliopita, ilifanikiwa kugawa chakula kwa watu 212,000 katika maeneo ya Magharibi na katika Bonde la Ufa/Rift Valley, pamoja na watu 160,000 waliopo katika jiji la Nairobi.

Sikiliza ripoti kamili, pamoja na mahojiano na Pamela Sittoni, Afisa wa Habari wa UNICEF, kwenye idhaa ya mtandao.