Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mchango wa UM kuhudumia amani na misaada ya kiutu Kenya

Mchango wa UM kuhudumia amani na misaada ya kiutu Kenya

Timu ya Mashirika Wakazi ya UM katika Kenya imeripoti hali, kwa ujumla, nchini, sasa hivi, inaendelea kuwa shwari na tulivu, isipokuwa katika miji ya Eldoret na Kericho ambako hali huko tumearifiwa bado ni ya kigeugeu na inatia wasiwasi.~

Mashirika ya UM, pamoja na yale yasiso ya kiserikali (NGOs), yameripoti kwamba matayarisho ya ardhi ya kilimo yamepwelewa kwa sasa kwenye Bonde la Ufa Kaskazini/Rift Valley, kabla ya kuwasili majira marefu ya mvua kuanzia mwezi Machi.

Mnamo mwanzo wa wiki, wahamiaji wa ndani ya nchi (IDPs) 11,000 waliopo Nakuru walifadhiliwa msaada wa tani za metriki 21 za chakula. Kadhalika, wahamiaji wa IDPs karibu 700 wa jimbo la Kati walitarajiwa kufadhiliwa misaada hiyo ya chakula. Halkadhalika, mapema wiki hii, malori 24 yaliyobeba shehena za chakula za tani za metriki 700 ziada, kutokea Bandari ya Mombasa yalianza misafara ya kupeleka misaada ya chakula katika sehemu kadha za Kenya na pia katika mataifa jirani ya Sudan, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Ofisi ya UM inayosimamia Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti kwamba machafuko yaliofumka Kenya baada ya uchaguzi yameipatia jumuiya kimataifa funzo maalumu kuhusu taratibu bora za kutekeleza, kwa haraka zaidi, zile huduma za dharura, kwa kulingana na mwongozo wa mfumo ulioanzishwa miaka miwili iliopita unaojulikana kama 'utaratibu wa mafungu' ambao hukabiliana na maafa ya dharura kwa kuwachangisha wadau wingi kikazi, kwa kuwagawa kwa mafungu mafungu kuhudumia miradi maalumu ya kusaidia waathiriwa wa maafa.

John Holmes, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) amesema atazingatia rai ya kuyaongezea majukumu mashirika yasio ya UM ili kuimarisha zaidi utekelezaji wa misaada ya kiutu kwa waathiriwa wa maafa.

Sikiliza kipindi kamili kwenye idhaa ya mtandao.