Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

KM na jamii ya kimataifa walaani mauaji ya wanajeshi wa AU Darfur

KM na jamii ya kimataifa walaani mauaji ya wanajeshi wa AU Darfur

KM Ban Ki-moon, akiungwa mkono na maofisa kadha wa vyeo vya juu katika UM, ameshtumu vikali mauaji ya wanajeshi wanaolinda amani wa Umoja wa Afrika Sudan (AMIS), yaliofanyika mwisho wa wiki iliopita katika mji wa Haskinita, Darfur Kusini.

Kwa mujibu wa taarifa za UM, wanajeshi karibu darzeni moja wa AMIS waliuawa na askari wengine kadha kujeruhiwa. KM alisema ameshtushwa na kitendo hicho alichokitafsiri cha “ukatili mkubwa”, na alihimiza juhudi za kuwasaka na kuwafikisha mahakamani wale walioendeleza jinao hiyo ziharakishwe. Mwenyekiti wa AU, Alpha Oumar Konare kwa upande wake alisema mashambulio haya ya “kuchukiza” yaliendelezwa na “watu waoga wasiopenda amani”, na aliwakumbusha wahalifu hawo ya kuwa AU “hautosita, asilan, katika kutekeleza ahadi ya kurudisha usalama na amani kwa umma wa Darfur.” Raisi wa Baraza la Usalama kwa mwezi Oktoba, Balozi Leslie Kojo Christian wa Ghana, aliripoti wajumbe wa Baraza “walichukizwa sana na mashambulio yaliosababisha vifo vya wanajeshi wa AU na kujeruhi askari kadha wengine na baadhi yao kutoweka." Baraza la Usalama pamoja na KM, na vile vile AU walituma rambirambi zao kwa Serekali za wanajeshi waathiriwa pamoja na kutoa mkono wa taazia kwa aila zao na masahibu.