Vijana wakutana Kampala kujadili amani na usalama- WFUNA
Hii leo huko Kampala Uganda, kunafanyika kongamano la kimataifa la vijana liilloandaliwa na shirikisho la kimataifa la jumuiya za Umoja wa mataifa, WFUNA.
Kongamano hilo la siku mbili linajadili changamoto na pia fursa katika ujenzi wa jamii zao kwa kuzingatia amani na usalama.
Wakati wa kongamano hilo washiriki watapata fursa za kujadili jinsi changamoto za amani na usalama zinavyoathiri jamii zao katika ulimwengu wa leo, katika ngazi za kitaifa na za kikanda kwa kutumia vipengele vya azimo namba 2250 la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa,
Pia watapata nafasi ya kujadili masuala ya usawa wa kijinsia , unyanyasaji wa kijinsia katika jamii ikiwa ni mipango ya utekelezaji wa azimio hilo.
Kongamano hili lenye lengo la kuwawezesha vijana kutoka mataifa mbalimbali kupata fursa ya kujifunza na kubadilisha mitazamo kuhusu suluhisho katika migogoro , litafika tamati kwa hotuba kutoka kwa Kessy Martine Ekomo-Soihnet ambaye ni mshauri wa vijana kitengo cha amani na usalama.