Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa Haki za Binadamu aisihi JKK kuwalinda mawakili, na watetezi wa haki za kiutu

Mkuu wa Haki za Binadamu aisihi JKK kuwalinda mawakili, na watetezi wa haki za kiutu

Navi Pillay, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu ametoa taarifa yenye kuihimiza Serikali ya JKK kuhakikisha mawakili na watetezi wa haki za binadamu, ikijumlisha waandishi habari, huwa wanapatiwa ulinzi unaofaa utakaowaruhusu kutekeleza majukumu yao, bila ya kuingiliwa kati kikazi wala kubaguliwa, kutishiwa au kulipizwa kisasi kwa sababu ya shughuli zao.

Taarifa hii ilijumlishwa kwenye ripoti iliotolewa bia na Ofisi yake pamoja na Shirika la UM Linalohudumia Ulinzi Amani katika JKK (MONUC) iliochapishwa Ijumanne. Ripoti ililenga juu ya namna utaratibu wa mahakama unavyoendeshwa nchini kufuatia mauaji ya 2007 ya Serge Maheshe, mwandishi habari mzalendo wa JKK aliyekuwa akitumikia UM. Miongoni mwa matokeo kuhusu uchunguzi juu ya mfumo wa mahakama katika JKK, ripoti ilieleza utaratibu wa kisheria nchini "ulikuwa na kasoro na hitilafu kadha wa kadha zenye kudhihirisha wazi kwamba jamii ya majaji hawataki au kutopendelea ukweli kujulikana" kuhusu mauaji ya mwandishi habari Maheshe.