Skip to main content

UM yahimiza Mataifa Wanachama yote kushirikiana kufyeka njaa duniani

UM yahimiza Mataifa Wanachama yote kushirikiana kufyeka njaa duniani

Josette Sheeran, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP), kwenye risala aliotoa mnamo siku ya pili ya Mkutano Mkuu wa Dunia juu ya Udhibiti Bora wa Akiba ya Chakula unaofanyika Roma, Utaliana, alisema raia wote wa kimataifa - na sio viongozi wa dunia pekee - wanawajibika kuhamasishwa wajitayarishe kuwapatia chakula watu bilioni moja ziada wenye kusumbuliwa na tatizo la njaa sugu ulimwenguni.

Alisema kudhaminia chakula kwa umma muhitaji katika dunia ni kitendo ambacho hakuhusiani na misaada ya kiutu na maendeleo ya kilimo pekee, bali vile vile hufungamana na utulivu, usalama na amani ya kitaifa, na ni suala la dharura liliokabili vizazi vya karne ya sasa hivi. Aliyahimiza mataifa yote, na umma wa ulimwengu kutumia rasilmali zote ziliopo kimataifa, kukomesha tatizo la njaa kote duniani.